Habari Mseto

Miezi mitatu wakiishi kichakani baada ya kukosa kodi

July 24th, 2020 1 min read

Na MWANDISHI WETU

MWANAMUME na mwanawe, ambao wamekuwa wakilala kichakani katika Kaunti ya Machakos, baada ya kutimuliwa kwa nyumba waliyokuwa wakiishi waliposhindwa kulipa kodi, walipokea msaada jana kutoka kwa wahisani.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Benjamin Kilonzo, alisema mambo yalimwendea mrama kufuatia janga la corona na akashindwa kumudu kulipa kodi ya nyumba.

“Nilikuwa nikifanya vibarua na kuuza kuni katika mikahawa na vibanda vya kuuzia chakula mjini Machakos, lakini vilipofungwa kwa sababu ya janga la corona, nilikosa mbinu ya kujipatia mapato,” alisema mwanamume huyo ambaye amedhoofika kiafya.

Alieleza kwamba baada ya kukosa kodi ya nyumba, landilodi alimfukuza na akawa hana pa kwenda. Picha/ Benson Matheka

Baada ya kukosa ajira na kufukuzwa nyumba aliyokuwa akiishi, alijaribu kumpeleka mwanae kwao Kangundo lakini jamaa zake walimrudisha mjini Machakos.

“Nilimtuma mwanangu nyumbani Kangundo akaishi na ndugu zangu lakini walikataa kumpokea na akarudi kuungana nami tena,” alisema.

Tangu wakati huo, wawili hao wamekuwa wakiishi kichakani katika mtaa wa Kathaayoni viungani mwa mji wa Machakos, ambapo ameunda makao kwa kutumia karatasi za plastiki na magunia.

Bw Kilonzo na mwanawe wa kidato cha pili wamekuwa wakilala kwenye godoro lililochanika wakivumilia baridi kali usiku.

Kwa miezi mitatu, hawajawahi kubadilisha nguo na huwa wanategemea chakula kutoka kwa wasamaria wema. Picha/ Benson Matheka

Jana wahisani waliwapa makao na pesa za matumizi baada ya masaibu yao kuangaziwa na vyombo vya habari.

Padri Lazarus Musyoka aliwapa nyumba ya kuishi, naye pasta Maurice Oloo akawapa Sh15,000 waanze maisha yao upya. Wahisani wengine pia waliwasaidia kwa vifaa mbali mbali vya matumizi.

“Mke wangu alitoroka na kuniachia mtoto huyo akiwa na miaka miwili. Nimefanya vibarua kumlea na kumsomesha hadi shule ya upili lakini corona imevuruga maisha yetu,” alieleza.