Makala

Paipu za maji safi zinazopitia kwenye mitaro ya majitaka huchangia kuenea kwa maradhi

November 6th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KWA muda wa miezi kadhaa Sarah Nduku, mkazi wa eneo la Zimmerman, Kaunti ya Nairobi amekuwa akipitia hali ngumu kufuatia maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.

Sarah ambaye ni mama wa mtoto mmoja amekuwa akimeza tembe za kuzima maumivu hayo.

Ni hali ambayo amekuwa akishuhudia asubuhi na jioni.

Alipotafuta ushauri wa kimatibabu, alihimizwa kufanya ukaguzi.

“Niligundulika kuugua Homa ya Matumbo. Daktari alinieleza kwamba ugonjwa huo ndicho kiini cha maumivu yangu ya kila mara,” anasema Sarah.

Kulingana na Dkt Job Mwangi, Homa ya Matumbo aghalabu husababishwa na maji na chakula, ikiwa hali yake si nzuri.

“Usafi wa maji na chakula na vifaa vya kuhifadhi unapaswa kuwa wa hadhi ya juu,” anasisitiza Dkt Mwangi.

Sarah anasema alikuwa na mazoea kunywa maji yatokayo kwenye mfereji bila ya kuchemsha au kuyatibu.

Kabla ahamie Zimmerman, hakuwa na tatizo lolote.

Eneo hilo, paipu nyingi za kusambaza maji imesindikwa kwenye mitaro ya majitaka, suala ambalo linatajwa kuwa kiini kikuu cha maradhi kama Homa ya Matumbo.

Kwenye uchunguzi wetu, tulibainisha sehemu nyingi zimeathirika; hasa Mirema, Base, Canopy, Kwa Wambuti, na zinginezo.

Taswira hiyo si tofauti na ya mtaa wa Githurai 44 na Kahawa West.

Majengo mengi katika mitaa hiyo ni ya vyumba vya kulipia kodi, na suala la majitaka limekuwa kero kuu.

Baadhi ya paipu za maji zimetoboka na wakati hayasambazwi bila shaka majitaka hupenyeza ndani.

“Nimeishi Zimmerman kwa zaidi ya miaka mitano, tatizo la paipu kuwa kwenye mitaro ya majitaka limekuwepo tangu awali,” akalalamika mkazi wakati wa mahojiano.

Alisema pia naye amewahi kuugua Homa ya Matumbo.

Maji yanayotumika Kaunti ya Nairobi na Kiambu husambazwa na kampuni ya Nairobi Water.

Kwenye mahojiano na mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo na aliyeomba jina lake lisichapishwe, amesema wamekuwa wakipokea malalamishi hayo.

“Tunapopokea malalamishi huyawasilisha katika kitengo kinachoshughulikia ukarabati wa mifereji na paipu,” akasema.

Uchafu wa kila aina

Majitaka yamekusanya uchafu wa kila aina, kuanzia kemikali inayotumika kwenye vyoo, kinyesi cha binadamu, na kemikali zinginezo.

Kulingana na Dkt Job Mwangi, uchafu huo ndio unasababisha magonjwa yanayohangaisha wakazi.

“Isitoshe, hali ya aina hiyo inawatia kwenye hatari kuugua Kipindupindu,” anaonya.

Mtaalamu huyo anatilia mkazo haja ya kuchemsha maji kabla ya kuyanywa na kufanya shughuli za mapishi. Hali kadhalika, anahimiza wakazi kuyatibu kwa dawa zilizopendekezwa, na ambazo pia huuzwa kwenye maduka ya kijumla.

Kuna dawa za tembe na za maji zinazotumika kutibu maji, kabla kuyatumia hasa kunywa au kufanya mapishi.

Mbali na kampuni inayojumika kusambaza maji, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa, zina wizara husika – ya afya na mazingira, zinazopaswa kuchukua hatua kuimarisha hali ya mazingira si tu katika maeneo yaliyoangaziwa ila yote yanayopitia hali hiyo. Vilevile, halmashauri ya kitaifa ya mazingira, Nema, inajumuishwa katika asasi husika kutathmini usalama wa mazingira.

Mitaa mingi katika kaunti ya Nairobi, kama vile Kariobangi, Mwiki, Mathare, Korogocho, Kibra, hiyo ikiwa michache tu kutaja, imeathirika kwa suala la maji na majitaka.