Michezo

Migne afafanua mbona akaacha 'Cheche' baridini

May 16th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

DAVID ‘Cheche’ Ochieng ni miongoni mwa wachezaji waliokosa kuunga orodha ya wanasoka 26 ambao kocha Sebastien Migne wa Harambee Stars atapania kuwategemea Juni 2019 katika kampeni za kuwania Kombe la Afrika (Afcon) nchini Misri.

Beki huyo matata wa AFC Leopards amekuwa na uhakika wa kuunga vikosi vyote ambavyo vimewahi kusukwa na Migne tangu alipokabidhiwa mikoba ya kuwanoa Stars mnamo Machi 2018.

Licha ya kuitwa kambini mwa Stars mara kwa mara, Cheche ambaye anajivunia utajiri mkubwa wa tajriba katika ulingo wa kimataifa, hajawahi kuwajibishwa katika mchuano wowote ndani ya jezi za timu ya taifa.

Badala yake, Migne amekuwa akitafadhalisha kuwachezesha mabeki Joash Onyango, Brian Mandela na Musa Mohammed katika safu ya kati ya ulinzi.

Akizungumza baada ya kukifichua kikosi chake kinachotazamiwa kuanza kujinoa kwa Afcon chini ya kipindi cha majuma mawili yajayo, Migne alielezea baadhi ya sababu zilizomfanya kuwatema baadhi ya wachezaji maarufu kikosini mwa Stars, huku akitetea maamuzi ya kuwaita kambini makipa wawili wa Kariobangi Sharks.

Mbali na Cheche, wengine waliotazamiwa kunogesha kampeni za timu ya taifa nchini Misri ni mvamizi Jesse Jackson Were wa Zeco United nchini Zambia na fowadi Dennis ‘The Menace’ Oliech wa Gor Mahia.

“Kuna baadhi ya wachezaji ambao nililazimika kuwapigia simu siku moja kabla ya kikosi cha Stars kwa minajili ya Afcon kufichuliwa. Niliteua kufanya hivyo (kuwaarifu kwamba hawataunga kikosi cha Stars) kwa sababu ya heshima yangu kwao,” akasema.

Akitumia mfano wa Cheche, Migne alikiri kwamba kiwango cha beki huyo katika mchuano wa mwisho uliomshuhudia akiwajibishwa na Leopards hakikumridhisha.

“Nilimtazama Cheche alipowajibishwa na waajiri wake katika safu ya kati. Alizidiwa maarifa kila alipohitajika kujituma zaidi na kuwania mipira ya juu. Nahisi kwamba bado hayupo tayari kukiwajibikia kikosi cha taifa,” akasema kocha huyo mzawa wa Ufaransa.

Cheche alikuwa miongoni mwa sajili wapya wa Leopards mnamo katika muhula mfupi uliopita wa usajili wa wachezaji baada ya kubanduka kambini mwa Brommapojkarna, Uswidi.

Licha ya kujivunia fomu ya kuridhisha kambini mwa Zesco na kuwa mfungaji bora wa kikosi hicho, Were aliyewahi kuvalia jezi za Tusker FC, pia aliachwa nje ya timu ya Stars.

Nyota huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji waliotemwa tena na Migne wakati alipokuwa akiandaa kikosi cha kuvaana na Ghana katika mechi ya marudiano ya kufuzu kwa fainali za Afcon.

Japo hakusafiri nchini Ghana, kujumuishwa kwake katika kikosi kilichojifua kwa minajili ya mchuano huo kulichochewa na jeraha alilolipata mvamizi Michael Olunga ambaye kwa sasa anawasakatia Kashiwa Reysol nchini Japan.