Michezo

Migne afurahia kuimarika kwa Harambee Stars

June 21st, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

CAIRO, Misri

KOCHA Sebastien Migne wa Harambee Stars amesema amefurahia kuimarika kwa wachezaji kufuatia maagizo yake kambini nchini Ufaransa.

Migne alieleza kuridhishwa na viwango vya wachezaji hao kambini, haswa walivyoshirikiana vyema katika mechi mbili za kupimana nguvu dhidi ya Madagascar na baadaye DR Congo ambazo matokeo yalikuwa 1-0 na 1-1 mtawalia.

“Nimefurahishwa na kuimarika kwa wachezaji kadhaa hasa Ayub Timbe ambaye ni mwepesi kushika filosofia yangu haraka, na iwapo ataendelea hivyo, bila shaka atakuwa mwanasoka hodari.”

Timbe ni miongoni mwa wachezaji walioeleza kuridhishwa na kambi ya makazi nchini Ufaransa huku akieleza jinsi walivyojiandalia katika mazingara mazuri.

“Ombi lango kwa Wakenya ni wazidi kutusapoti kwa sababu naamini tutawashangaza wengi waliotupuuza,” alisema Timbe.

Timbe ambaye hucheza soka ya kulipwa nchini China ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kung’ara baada ya ndoto yake ya miaka mingi kutimia.

Harambee Stars wamepangwa katika Kundi C ambalo linajumuisha timu za Algeria, Senegal na majirani Tanzania, timu ambazo zimebeba mastaa kadhaa wanaosakatia klabu kubwa duniani.

Nyota hao ni pamoja na Sadio Mane wa Liverpool, Diara Sakho wa West Ham United na Pepe Abou Cisse miongoni mwa wengine.

Kadhalika kutakuwa na Riyad Mahrez (Manchester City), Yacine Brahimi (FC Porto, Ureno), Aissa Mandi (Real Beits, Uhispania), Mehdi Zeffane (Rennes, Ufaransa), Mehdi Tahrat (Lens, Ufaransa), Sofiane Feghouli (Galatasaray, Uturuki).

Nyota chipukizi

Tanzania kwa upande wake inajivunia nyota kadhaa chipukizi wanaotarajiwa kuzua upinzani mkali. Pia kuna mkali Mbwana Ally Samatta wa Genk ya Ubelgiji pamoja na kinda mahiri, Kelvin John ‘Mbappe’.

Mashabiki wa soka nchini hapa wamemlaumu kocha Sebastien Migne kwa kuwaita washambuliaji watatu pekee kwenye kikosi chake cha wanasoka 23.

Kutokana na hatua hiyo, mashabiki wanadhania kuwa huenda nia yake ni kucheza mchezo wa kulinda zaidi katika mechi za AFCON.

“Mimi sipangi kuweka basi. Mfumo wangu ni kuhakikisha tunalinda vizuri na kushambulia kama timu. Tunatakiwa kuwa sawa katika safu ya ulinzi ili kuepuka kuruhusu mabao ya rahisi kuingia langoni mwetu,” alisema Kocha Migne

Stars wataanza na Algeria mnamo Juni 23.