Michezo

Migne ataka Stars kuwa macho dhidi ya Tanzania CHAN

July 24th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Sebastien Migne amewakata masogora wake wa Harambee Stars kujihadhari zaidi dhidi ya Tanzania watakapokutana katika mchujo wa kufuzu kwa fainali za CHAN 2020.

Migne anahisi kwamba Tanzania itapania kuwajibisha wachezaji walio na tajriba na uzoefu mpana zaidi katika kivumbi hicho cha Julai 28.

Wakifichua kikosi chao kwa minajili ya mechi dhidi ya Kenya, Tanzania walidumisha wengi wa masogora waliowategemea katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizokamilika nchini Misri majuzi.

Kati ya wachezaji 23 waliounga kikosi kilichopeperusha bendera ya Tanzania katika makala hayo ya 32 ya AFCON, 10 wamehifadhi nafasi zao katika timu ambayo kwa sasa inajiandaa kuvaana na Kenya.

Hao ni pamoja na kipa Aishi Manula, Metacha Mnata, David Mwantika, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Yahya Mudatiri, John Bocco, Feisal Salum, Frank Domayo na Gadiel Michael.

CHAN ni kivumbi ambacho huwajumuisha wachezaji wanaonogesha kampeni za ligi zao za nyumbani pekee.

“Kipute dhidi ya Tanzania kitakuwa kigumu. Wengi wa wachezaji waliowategemea katika fainali za AFCON ni wale wanaoshiriki ligi yao ya nyumbani. Isitoshe, wanajivunia tajriba pevu katika majukwaa ya kimataifa,” akasema Migne.

Ingawa hivyo, mkufunzi huyo mzawa wa Ufaransa amesisitiza kwamba anaridhishwa na kiwango cha wachezaji ambao amewaita kambini na kufichua kwamba wana uwezo wa kuwatatiza wapinzani wao jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii.

Kufikia mwisho wa wiki jana, Migne alikuwa na wachezaji 23 kati ya 27 aliowaita kambini kwa minajili ya kujifua kwa mechi dhidi ya Tanzania. Kikosi cha Stars kinajiandalia uwanjani MISC Kasarani.

Awamu ya makundi Afcon 2019

Akidhibiti mikoba ya Stars nchini Misri, Migne aliwaongoza vijana wake kupepeta Tanzania 3-2 katika mojawapo ya mechi za Kundi C kwenye AFCON 2019.

Kenya itakuwa ikitafuta ushindi wa pili mfululizo mwaka huu dhidi ya majirani zake hao, kisha kujikatia tiketi ya kunogesha fainali za CHAN kwa mara ya kwanza katika historia Ya michuano hiyo.

Baada ya Kenya kupimana ubabe na Tanzania katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Julai 28, vikosi hivyo vitarudiana ugani Kasarani mnamo Agosti 4.

Mshindi baada ya michuano hiyo ya mikondo miwili atafuzu kumenyana na Sudan katika raundi ya pili na ya mwisho ya mchujo. Kenya ikipiga Tanzania na Sudan, itajikatia tiketi ya kushiriki kivumbi cha CHAN kitakachoandaliwa nchini Cameroon mnamo Januari 2020.

Ethiopia waliokuwa wamefuzu moja kwa moja kunogesha makala hayo ya sita ya CHAN mwakani kabla ya kupoteza haki na fursa ya kuyaandaa, wameratibiwa kuvaana na Djibouti ambapo mshindi baada ya michuano mingine ya mikondo miwili atapepetana na Rwanda ili kufuzu kwa fainali.

Mshindi kati ya Burundi/Sudan Kusini na Somalia/Uganda pia atafuzu kushiriki mashindano haya yatakayoleta pamoja mataifa 16 ya Afrika.

Kikosi cha Harambee Stars:

Makipa: John Oyemba (Kariobangi Sharks), James Saruni (Ulinzi Stars).

Mabeki: Philemon Otieno (Gor Mahia), Yusuf Mainge (AFC Leopards), Joash Onyango (Gor Mahia), Benard Ochieng (Wazito), Mike Kibwage (KCB), Andrew Juma (Mathare United), David Owino (Mathare United)

Viungo: Dennis Odhiambo (Sofapaka), Teddy Osok (Wazito), Kenneth Muguna (Gor Mahia), Duke Abuya (Kariobangi Sharks), Patillah Omoto (Kariobangi Sharks), Paul Were (AFC Leopards), Samuel Onyango (Gor Mahia), Roy Okal (Mathare United), Whyvone Isuza (AFC Leopards), Abdalla Hassan (Bandari), Ibrahim Shambi (Ulinzi Stars).

Wavamizi: John Avire (Sofapaka), Musa Masika (Wazito), Nicholas Kipkirui (Gor Mahia), Sydney Lokale (Kariobangi Sharks), Piston Mutamba (Wazito), Enosh Ochieng (Ulinzi Stars), Derrick Otanga (Wazito).