Michezo

Migne atemwe asitemwe, mjadala wapamba moto baada ya kipigo

June 24th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MWAKA mmoja na miezi miwili baada ya Sebastien Migne kuajiriwa na Kenya kunoa Harambee Stars kwa kandarasi ya miaka mitatu, baadhi ya mashabiki wa Kenya wanataka apigwe kalamu.

Hii ni baada ya kocha huyu Mfaransa, ambaye ni mara yake ya kwanza kuongoza timu kwenye Kombe la Afrika (AFCON) kuonjeshwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Desert Warriors.

Baghdad Bounedjah na Riyad Mahrez walifungia Algeria mabao hayo katika dakika ya 34 na 43 mtawalia.

Shabiki Ezekiel Bor Chiroch alisema, “Ambieni kocha wa Harambee Stars asirudi Kenya; alikuwa na mapendeleo wakati wa kuchagua kikosi chake ambacho sasa kinatuumiza.”

Naye Carsonb Turan Gacheru alisema, “Migne anafaa kutimuliwa Kenya kabla hata ya AFCON kumalizika.”

Robert Ouma amelaumu Migne akisema, “Kocha alifanya makosa katika kuchagua kikosi chake pamoja na kuchagua kikosi kilichoanza mechi…”

Warren Wambua aliuliza swali la kizushi baada ya Kenya kuenda mapumzikoni ikiwa nyuma mabao mawili. “Inawezekana yupiga kalamu kocha timu wakati wa mapumziko?”

Hawa ni sehemu ndogo ya mashabiki walioelekeza lawama zao kwa kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Congo Brazzaville.

Mashindano makubwa kama AFCON, Kombe la Dunia, Kombe la Bara Asia, Copa Amerika, Olimpiki na Kombe la Bara Ulaya huwa katili kwa makocha. Haitastaajabisha kuona baadhi ya makocha wakiangukiwa na shoka baada ya makala ya 32 ya AFCON yanayoendelea nchini Misri.

Migne aliajiriwa na Kenya mnamio Mei 3 mwaka 2018. Alisaidia Kenya kurejea katika AFCON baada ya kuwa nje miaka 15.

Kutokana na mafanikio, hatarajiwi kutemwa pengine Kenya ikilenga hata kumuongeza muda kuona kama ataiwezesha kuingia makala ya mwaka 2021 nchini Cameroon na Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.

Mashabiki wengi wa Kenya wanaunga mkono Migne, ambaye mara kwa mara amekuwa akitisha kujiuzulu baada ya mshahara wake kucheleweshwa.

Tayari kocha kutoka Mexico Javier Aguirre ametangaza kwamba atajiuzulu asipoongoza wenyeji Misri kushinda mashindano haya ya mataifa 24. Mafirauni wa Misri ndio wanashikilia rekodi ya mataji mengi. Wana mataji saba, ingawa mara ya mwisho walishinda ni mwaka 2010.

Kenya iko katika Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Tanzania. Harambee Stars italimana na Tanzania mnamo Juni 27, mechi ambayo Wakenya wanatarajiwa kuongeza sauti kuhusu mjadala wa Migne kutemwa asipopata ushindi. Itakamilisha mechi za makundi dhidi ya Teranga Lions mnamo Julai 1.