Michezo

Migne kutaja kikosi cha Stars tayari kwa Afcon

May 14th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MWEZI mmoja baada ya Kenya kufahamu wapinzani wake wa mechi za makundi za Kombe la Afrika (Afcon), kocha Sebastien Migne atatangaza leo Jumanne kikosi kitakachopeperusha bendera nchini Misri hapo Juni 21 hadi Julai 19, 2019.

Harambee Stars, ambayo inarejea katika kombe hili baada ya kukosa makala saba yaliyopita, itaelekea nchini Ufaransa Mei 31 kwa kambi ya mazoezi.

Wakiwa jijini Paris, vijana wa Migne watamenyana na Madagascar hapo Juni 7 na Gambia hapo Juni 15 katika mechi za kirafiki.

Watasafiri hadi Misri kwa fainali hizo Juni 19.

Katika Afcon, Kenya inayojivunia nyota Victor Wanyama anayesakatia Tottenham Hotspur, itakabiliana na Algeria (Juni 23), Tanzania (Juni 27) na Senegal (Julai 1) katika Kundi C Juni 30 jijini Cairo.

Huku Wakenya wakisubiri kadi za Migne, tovuti ya Africa Top Sports iliripoti Mei 12 kwamba Aliou Cisse atataja kikosi cha Senegal cha wachezaji 27 Mei 20.

Senegal, ambayo inajivunia kuwa na mkali wa Liverpool, Sadio Mane, itafanyia mazoezi nchini Uhispania. Itapimana nguvu dhidi ya Super Eagles ya Nigeria hapo Juni 16.

Algeria anayochezea nyota wa Manchester City, Riyad Mahrez, haijaanika mipango yake.

Kocha wa Tanzania, raia wa Nigeria, Emmanuel Amuneke alitangaza kikosi cha wachezaji 39 hapo Mei 2.

Matayarisho makali ya Tanzania yataanza mapema Juni nchini Misri. Itapimana nguvu na Misri Juni 13.

Maoni ya baadhi ya Wakenya

Droo ya Afcon ilipofanywa Aprili 12 jijini Cairo, Wakenya walikuwa na maoni mbalimbali kuhusu hatima ya Stars kundini.

Wengi waliamini vijana wa Migne wanaweza kuzima wapinzani wake hao na kuingia raundi ya 16-bora, huku sehemu nyingine ikisalimu amri mapema.

Si siri kwamba kibarua kitakuwa kigumu kwa Kenya, ambayo mara ya mwisho ilishiriki AFCON ni mwaka 2004 nchini Tunisia. Mwaka huo pia ndio ulikuwa wa mwisho Stars kukutana na Senegal na iliadhibiwa 3-0 katika mechi za makundi.

Rekodi ya Kenya dhidi ya Algeria na Tanzania inatia moyo, ingawa wapinzani hawa hawawezi kupuuzwa. Migne hatarajiwi kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi kilichoshiriki mechi za kufuzu kati ya Juni mwaka 2017 na Machi 2019.

Mshambuliaji wa klabu ya Kashiwa Reysol, Michael Olunga, ambaye aliongoza kufungia Kenya katika safari yake ya kurejea Afcon, pamoja na kiungo nyota wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama ni baadhi ya ‘vifaa’ Migne atatumai watakuwa fiti kuongoza kampeni yake nchini Misri.

Winga matata Ayub Timbe anayesakata soka Uchina anatarajiwa kurejea kikosini baada ya kukosa mechi mbili dhidi ya Ghana na idadi sawa dhidi ya Ethiopia katika mechi za kufuzu akitumikia marufuku aliyopata dhidi ya Sierra Leone mnamo Juni 10 mwaka 2017.