Makala

Migogoro ya ardhi yapungua tangu kitabu kuanika makateli

February 25th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

MIGOGORO kuhusu suala tata la ardhi katika Kaunti ya Lamu imepungua pakubwa tangu kuzinduliwa kwa kitabu maalumu kilichoweka wazi sababu zinazochangia mizozo hiyo.

Kitabu hicho kinachoenda kwa kichwa ‘Excluded and Displaced in Your Own Homeland’ kilizinduliwa Lamu mnamo Machi 24, 2023.

Kinajadili na kuchambua kwa kina dhuluma za kihistoria, ukosefu wa haki na mizozo inayozunguka na kufungamana na suala zima la ardhi kote Lamu.

Isitoshe, mwandishi wa kitabu hicho, wakili George Wakahiu, pia anachambua baadhi ya mambo makuu yanayoaminika kuchangia utata wa ardhi na hata kutoa mapendekezo ya jinsi matatizo hayo yanavyoweza kushughulikiwa na taasisi husika za serikali na jamii ili kumaliza zogo la ardhi.

Wakili George Wakahiu, mwandishi wa kitabu cha masuala ya ardhi chenye anwani ‘Excluded and Displaced in Your Own Homeland’. Miongoni mwa masuala aliyochambua na yanayoaminika kuleta migogoro ya ardhi Lamu ni jinsi wenyeji kindakindaki wanavyokosa haki ya kumiliki ardhi. Anasema ni asilimia 20 pekee ya wakazi walio na hatimiliki kwa vipande vyao vya ardhi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kitabu hicho pia kinafichua jinsi serikali kuu inavyotwaa ardhi za wenyeji kwa minajili ya kuanzisha au kuendeleza miradi mikuu na kisha kukosa kuwafidia waathiriwa kikamilifu.

Suala la wenyeji kindakindaki wa Lamu kukosa hatimiliki za ardi pia linagusiwa kwenye kitabu hicho, ambapo utafiti uliofanywa na mwandishi na taasisi tofautitofauti unabaini kuwa ni asilimia 20 pekee ya wenyeji wa Lamu ambao wana hatimiliki kwa ardhi zao.

Ni kutokana na chambuzi zilizomo kwenye kitabu hicho ambapo wakazi waliohojiwa na Taifa Jumapili walikiri kwamba kimesaidia kuleta afueni.

Bi Amina Athman, mkazi wa Mokowe, anasema kuchapishwa kwa kitabu hicho kumewazindua wengi kutoka usingizini.

Bi Athman anasema siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa pilkapilka za serikali kuu, ile ya kaunti na hata Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) katika kushughulikia migogoro ya vipande vya ardhi Lamu.

“Twashukuru kuchapishwa, kuzinduliwa na kusambazwa kwa nakala za kitabu hiki cha ‘Excluded and Displaced in Your Own Homeland’. Tangu kutolewa kwake, tumejionea mawaziri wa Ardhi na Usalama wa Ndani wa serikali kuu wakija Lamu mara kwa mara kutaka kujua ni vipi suala la ardhi na duluma nyinine za kiistoria zinesuulikiwa na kutatuliwa ipasavyo,” akasema Bi Athman.

Naye Bw Mohamed Omar, mkazi wa kisiwa cha Lamu, anasema kuzinduliwa kwa kitabu hicho pia kumepunguza presha miongoni mwa wananchi kwani hata maandamano ya kila mara ya waliojidai kuwa maskwota Lamu yamepungua.

“Kitabu kimeorodhesha kwa ustadi kipasacho kutekelezwa, iwe ni kwa upande wa jamii, taasisi za serikali na wadau wengine katika kukabiliana na utata wa ardhi za Lamu. Ndio sababu utaona hata wale waliokuwa wakiandamana bila mpangilio wakidai ni maskwota na wangetaka haki itendeke kwao pia wamelegeza kamba siku hizi. Hawamo tena barabarani baada ya kupitia kwa makini chapisho la kitabu hicho,” akasema Bw Omar.

Mbali na migogoro ya ardhi, pia kumeshuhudiwa amani na utulivu wa ali ya juu Lamu kinyume na nyakati kabla kitabu kuzinduliwa.

“Watu walijisomea nakala ya kitabu na kupata kufahamu chimbuko la mizozo inayowakumba ya ardhi. Kitabu kimewafunza wakazi kuhusu haki na jinsi wanavyoweza kuitafuta na kuipata kwa njia ya amani na utulivu,” akasema Bi Susan Mwoki, mkazi wa Hindi.

Abdallah Ali, mvuvi, anasema ni kupitia kusambazwa kwa kitabu hicho ambapo kaunti imejikaza kuwasaidia wavuvi wa sehemu mbalimbali za Lamu kukomboa ardhi zao za magegesho ya wavuvi ambazo awali zilikuwa zimenyakuliwa au kutwaliwa na watu binafsi.

“Niko na imani kubwa kwamba kitabu kilileta msukumo na mihemko kwenye idara mbalimbali, hivyo watu kuwajibika vilivyo. Nina furaha kuona hata kaunti yetu ikiwajibikia vilivyo suala la ardhi za maeneo yetu kama wavuvi na kuzikomboa,” akasema Bw Ali.

Kitabu hicho kilichochapishwa chini ya mwavuli wa Shirika la Haki Yetu pia kilitaja Kiunga, Faza, baadhi ya maeneo ya Hindi, Kisiwa cha Manda, Witu na Bahari kuwa miongoni mwa maeneo ambapo ardhi zipo lakini hazijasajiliwa na wenye ardhi hizo kukabidiwa hatimiliki, hivyo kuchangia migogoro isiyoisha ya ardhi Lamu.

Meneja anayeshughulikia mipango wa Shirika la Haki Yetu, Bw Peter Kazungu anaamini kuwa endapo mapendekezo yote yaliyoorodheshwa kwenye kitabu hicho yatafuatwa kikamilifu, utata wa ardhi na mizozo ya kila mara Lamu itazikwa katika kaburi la sahau.

“Ujio wa miradi mikuu kaunti ya Lamu, ikiwemo ule wa Sh310 bilioni wa Bandari ya Lamu umechangia pakubwa watu kupenda kuingia na kuish Lamu, hivyo kuleta mizozo isiyoisha ifungamanayo na ardhi. Ninaamini mapendekezo ya kitabu endapo yatazingatiwa vilivyo hii mizozo itakoma kabisa,” akasema Bw Kazungu.

Waziri wa Ardhi wa Kaunti ya Lamu, Tashrifa Bakari Mohamed akidurusu kitabu kwa jina ‘Excluded and Displaced in Your Own Homeland’. PICHA | KALUME KAZUNGU