Michezo

Migogoro ya Barcelona yamshangaza Messi

February 21st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BARCELONA, Uhispania

LIONEL Messi ameelezea “kushangazwa” na kitendo cha klabu yake ya Barcelona kuvutana na kampuni inayosemekana kuwakosoa vikali wachezaji wa sasa na wa zamani wa klabu hiyo, kwenye mitandao ya kijamii.

Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu alisema Jumanne kuwa klabu hiyo imekatiza kandarasi yake na kampuni ya I3 Ventures, ambayo ilikuwa imepatiwa kazi ya kupepeta sifa za Bartomeu na bodi ya klabu hiyo mitandaoni.

Kwa mujibu wa redio ya Cadena Ser Catalunya nchini Uhispania, kampuni hiyo ilisimamia akaunti kochokocho zilizokosoa wachezaji Messi, Gerard Pique, Xavi Hernandez, Pep Guardiola na Carles Puyol kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter.

Miongoni mwa jumbe zilizotajwa na ripoti hiyo ni moja iliyotoa hisia kali dhidi ya straika Messi kuchelewa kusaini kandarasi mpya.

Ujumbe mwingine ulipinga Pique kujihusisha na mashindano ya tenisi ya Davis Cup.

“Ukweli ni kuwa nashangazwa kwamba kitu kama hiki kinafanyika,” Messi alisema kwenye mahojiano yaliyochapishwa hapo jana na gazeti la Mundo Deportivo.

“Hata hivyo, walisema pia kutakuwepo na ushahidi. Tutasubiri kuona kama kile wanachosema ni kweli ama uongo.

“Hatuwezi kusema mengi. Wacha tusubiri kitakachofanyika. Ni kitu kinachoshangaza,” aliongeza nahodha huyo wa Barca.

Bartomeu amekutana na wachezaji wazoefu akiwemo Messi kuwapa maelezo dhahiri.

Siku ya Jumatatu, klabu ya Barca ilitoa taarifa kuwa haikuhusika katika kutoa jumbe hizo.

Rais Bartomeu alitilia mkazo msimamo huo hapo Jumanne.