Habari Mseto

Migogoro ya unyakuzi wa ardhi Pwani yazua hofu  

February 25th, 2024 1 min read

NA WINNIE ATIENO

SENETA wa Mombasa, Bw Mohammed Faki ameisihi serikali kuu ikabiliane na changamoto ya unyakuzi wa ardhi eneo la Pwani.

Bw Faki alitaja unyakuzi huo kuwa janga kuu ambalo linafaa suluhu ya kudumu.

Akiongea Jumamosi, Februari 24, 2024 kwenye mkutano wa wanakamati wa mashamba ya Gandini, Maunguja, na Kashani, Seneta Faki, alisema suala la unyakuzi wa ardhi ni la jadi.

“Suala la unyakuzi wa mashamba ni la kihistoria hasa hapa Mombasa ambapo wakazi wengi wanakodolea macho ufurushwaji na wengine hata kufurushwa,” alisema.

Bw Faki alisisitiza migogoro kati ya wamiliki wa mashamba na wakazi inafaa kutatuliwa.

“Tutashirikiana ili kuleta mwafaka kati ya wamiliki wa majumba hayo na wakazi,” aliongeza.

Alisema atashirikiana na vyombo vya serikali kutatua changamoto hiyo.