Migomo shuleni itafutiwe suluhu

Migomo shuleni itafutiwe suluhu

Na MHARIRI

MIGOMO ya wanafunzi wa shule za upili ambayo hushuhudiwa kila mwaka inafaa kusuluhishwa.

Kila mara wanafunzi hao wanapogoma, wadau huanza kutoa maoni yao kuhusu kile ambacho kinadhaniwa kuwa chanzo cha migomo hiyo ila bado hutokea.Mojawapo ya masuala ambayo hutajwa kuaminika kuchangia wanafunzi kugoma ni ukosefu wa ushauri nasaha, wanafunzi kutoadhibiwa ipasavyo wanapokosea, na pia kutosikilizwa kwa wanafunzi ambao huenda wakawa wanapitia changamoto zinazoweza kutatuliwa kabla wasababishe migomo.

Migomo aina hii ambayo husbaabisha uharibifu wa mali shuleni na hata imewahi kusababisha maafa na majeraha ya wanafunzi, imekuwepo tangu jadi.Ingetarajiwa kuwa, kufikia wakati huu, wadau wangekuwa wamejifunza kuhusu masuala ambayo huenda yakawa ni kiini chao.

Visababu ambavyo hutolewa na wanafunzi wanapogoma, kama vile kukatazwa kutazama runinga, kunyimwa nafasi ya kutangamana na wenzao wa jinsia tofauti, kutopewa chakula cha kutosha au kupikiwa chakula kibovu, uoga wa mitihani, miongoni mwa vingine huwa havina msingi.

Hii ni kutokana na kuwa, wasimamizi wa shule mbalimbali wamefanikiwa kutatua baadhi ya malalamishi aina hii katika miaka iliyopita ila bado migomo yatokea.Vile vile, kama ni kuadhibiwa, kuna hata wanafunzi ambao hufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa kushiriki migomo ambayo husababisha uharibifu wa mali na kudhuru maisha ya wenzao ila bado wanafunzi hawashiki adabu.

Wakati huu, kunao wanaoamini kuwa migomo inayoshuhudiwa sasa imetokana na kuwa mihula imefuatana kwa karibu kwa sababu ilitatizwa na janga la virusi vya corona.

Inaaminika hali hii imewasababisha watoto kuchoka, ilhali muhula huu hautarajiwi kuwa na kipindi cha mapumziko ya katikati ya muhula. Kimsingi, sababu zote hizi ambazo hutajwa mara kwa mara zafaa kuangaliwa kwa pamoja ili suluhisho ipatikane mara moja.

Bila hili, wadau watazidi kujikita katika kutatua dhana pekee huku mizizi ya migomo ya wanafunzi ikizidi kuenea miongoni mwao.Ikiwa tatizo ni mbinu za usimamizi wa shule, basi pia walimu wapewe mafunzo upya kuhusu jinsi wanavyofaa kubadili mitindo yao kwa manufaa ya jamii yote.

You can share this post!

Gavana abuni jopokazi kuchunguza madai hatari kuhusu visa...

Kebs na Inable wazindua kanuni za kuwafaa walemavu...

F M