Makala

MIGORI: Ayacko kutolewa jasho na limbukeni wa miaka 27 ni ishara kuwa Raila ameisha makali

October 13th, 2018 4 min read

Na CHARLES WASONGA

JAPO ilitarajiwa kuwa mgombeaji wa chama cha ODM Ochilo Ayacko angeibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Migori uliokamilika Jumatatu, ushindi huo haukuwa rahisi ingawa kaunti hiyo ni ngome ya ODM.

Mahasidi na wafuasi na mahasidi wa chama hicho kinachoongozwa na kiongozi wa upinzani walishangazwa na ushindani mkali alioupata kutoka kwa mwanasiasa chipukizi Eddy Oketch mwenye umri wa miaka 27.

Mwanasiasa huyo aliwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Federal Party of Kenya alipata kura 60,555 nyuma ya Bw Ayacko ambaye alipata kura 85,234, pengo kati yao ikiwa kura 24,679 pekee!.

Bw Oketch alionekana kuchangamkia matokeo hayo akisema kuwa yanaashiria kuwa nyota yake inazidi kung’aa zaidi. Na kinyume cha matarajio ya wengi, alizinguka katika maeneo bunge yote nane kwa helikopta akiwashukuru wapiga kura kwa kumuunga mkono, hata kabla ya Bw Ayacko kufanya hivyo.

Matokeo haya yamezua mdahalo mkubwa nchini huku mahasidi wa kiongozi wa ODM Raila Odinga walibashiri kuwa yanaashiri kudidimia kwa ushawishi wake katika ngome yake ya Luo Nyanza.

“Nilishangaa, sawa na wadadisi wengine wa kisiasa Kenya. Ni vipi limbukeni mwanasiasa mchanga mwenye umri wa miaka 27 aliweza kumtoa jasho mwanasiasa mkongwe kama Raila Odinga, tena katika ngome yake? Huu ushindi mwembamba wa Bw Ayacko unaaonyesha kuwa Baba ameisha makali na anafaa kustaafu kutoka siasa,” anasema kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen.

Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet aliongeza kuwa matokeo hayo yalimwaibisha kiongozi huyo wa upinzani machoni kwa wafuasi wake na Wakenya kwa jumla ikizingatia kuwa yamejiri miezi kadhaa baada yake kutia saini muafaka wa maelewano na Rais Uhuru Kenyatta.

Hata hivyo, wandani wa kinara huyo wa upinzani wanapuuzilia mbali madai hayo na huku wakisema matokeo hayo yalithibitisha tu kuwa Bw Odinga bado ndiye “mfalme wa siasa” katika Luo Nyanza.

“Ningependa kuwahikikishia wafuasi wa chama chetu na ODM kwamba chama hicho hakikabiliwi na tisho lolote katika kaunti ya Migori na maeneo mengine nchini. Na ushindi wa Mheshimiwa Ayacko ilithibitisha ukweli huo licha ya maadui wetu kumfadhili kijana Eddy Oketch,” anasema kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa bunge la kitaifa John Mbadi.

“Ni kweli kwamba tulikabiliwa na upinzani mkali lakini hatimaye tulishinda kwa sababu hatukuwachukuliwa wapinzani wetu ingawa baadhi yao walidhaminiwa na wapinzani wa kiongozi wetu katika ngazi ya kitaifa,” akaongeza Mbunge huyo wa Suba Kusini.

Mbadi anaonekana kukariri madai ya wenzake waliodai kuwa Bw Oketch alipata ufadhili kutoka kwa Naibu Rais William Ruto, madai ambaye mgombeaji huyo wa Federal Party of Kenya aliyakana vikali.

Mwanasiasa wa eneo la Homa Bay Tom Alila anasema ushindi mwembamba wa Bw Ayacko ambaye amehudumu kama mbunge wa Rongo na waziri wa Kawi, ulitokana na hali kwamba uteuzi haufanywa kwa njia iliyowaridhisha wafuasi wa ODM katika kaunti ya Migori.

“Itakumbukwa kuwa mgombeaji huyo alipewa tiketi ya moja kwa moja baada ya ODM kudai kuwa ilifanya kura ya maoni na kubaini kuwa ndiye alikuwa maarufu zaidi. Hatua hiyo ilipingwa vikali na wafuasi wa ODM akiwemo Gavana Okoth Obado. Hii ndio ilikasirisha wapiga kura kiasi kwamba wengi wao walichelea kujitokeza au wakaamua kumpigia kura kijana Oketch,” Bw Alila alinukuliwa akisema.

Huenda hii ndio maana ODM ilipong’amua ingepoteza, kamati iliyoongoza kampeni za Bw Ayacho ikiongozwa na Mbunge wa Suna Mashariki ililazimika kuomba msaada kutoka kwa Bw Odinga dakika za mwisho

Bw Odinga alipiga kambi katika kaunti ya Migori kwa siku mbili mfulululizo akimpigia debe Bw Ayacko katika maoeneo bunge ya kaunti hiyo. Hata hivyo, alishindwa kupenya katika maeneo bunge ya Kuria Mashariki na Kuria Magharibi kutokana na kile kilichotajwa kama “sababu za kiusalama”.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora anasema kuwa ODM iliamua kuingiza jina la Naibu Rais Bw Ruto katika kampeni hizo baada ya kung’amua kuwa “maji ilikuwa imezidi unga” na ushinde ulikuwa ikinukia.

“Mbinu hii ambayo ODM ilikumbatia dakika za mwisho ndio iliokoa jahazi lake ambalo lilikuwa likiendelea kuzama. Wapanga mikakai wa chama hicho walifanya hivyo ili kuvutia wapiga kura wengi upande wa Bw Ayacko ikizingatiwa kuwa Bw Ruto sasa ndiye hasidi mkubwa wa Bw Odinga katika siasa za ngazi ya kitaifa,” anasema.

“Kwa hivyo walinadi dhana kwamba uchaguzi huo mdogo wa useneta wa Migori ulikuwa ni ushindani kati ya Bw Odinga na Naibu Rais, ikizingatiwa kuwa wawili hao wanakimezea mate kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2022,” anaongeza Profesa Manyora ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Sawa na Bw Murkomen, Profesa Manyora anasema matokeo hayo yaliyotoa taswira kwamba huenda ushawishi wa ODM na Bw Odinga, unadidimia katika ngome yake ya Luo Nyanza.

“Huenda kivumbi kikali kingeshuhudiwa katika uchaguzi huo mdogo endapo Gavana Obado angekuwa huru na kupata nafasi ya kuendesha kampeni za kumpinga Bw Ayacko ikizingatiwa kuwa kiongozi huyo amewahi kukaidi chama hicho na kushinda kwa tiketi ya chama kisicho na umaarufu eneo hili, People’s Democratic Party (PDP),” anaeleza.

Lakini mchanganuzi wa siasa za eneo hilo Bw Odoyo Owiti anasema japo wakazi wa Migori wamewahi kumkaidi Bw Odinga katika chaguzi za vit vingine, wakazi hao humpa Odinga “kura zote za urais”.

“Kwa hivyo, umaarufu wa Odinga bado uko imara katika kaunti ya Migori. Hata hivyo, chama hicho kinapasa kuhakikisha kuwa haki inazingatiwa wakati wa uteuzi wa wagombeaji wake. Hii ni kwa sababu Migori ni kando na Obado aliyekuwa Mbunge wa Awendo James Opiyo alishinda kiti cha ubunge cha Migori kwa tiketi ya Ford Kenya baada ya kutendewa hiana katika kura ya mchujo,” anasema Bw Owidi ambaye ni mwenyiti wa Luo Dialogue Initiative.

Kwa upande wake, Bw Junet, ambaye ni kiranja wa wachache katika bunge la kitaifa anasema Migori bado ni ngome ya ODM huku akipuuzi dhana kuwa “imevamiwa na vyama pinzani”

“Watu hawakujitokeza kwa wingi kwa sababu uchaguzi huo mdogo ulifanyika siku ya Jumatatu siku ya kazi. Hii ndio maana kati ya jumla ya wapiga kura 388,633 ni wapiga kura 150,678 pekee waliojitokeza kupiga kura,” anasema.