Habari MsetoSiasa

MIGORI: Wafanyakazi hewa wamekuwa wakinyonya Sh10m kila mwezi

July 16th, 2018 1 min read

Na Vivere Nandiemo

KAUNTI ya Migori imekuwa ikipoteza zaidi ya Sh10 milioni kwa mishahara ya wafanyakazi hewa kila mwezi. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na Gavana Okoth Obado wiki iliyopita.

Kulingana na ripoti hiyo, serikali ya kaunti imekuwa ikilipa mishahara ya Sh327,790 kila mwezi kwa watu watatu ambao walikuwa wamejiuzulu, na Sh114,205 kwa watu wawili ambao walikuwa wamesimamishwa kazi.

Kwa jumla, kulikuwa na wafanyakazi 50 ambao waliacha kazi ilhali walikuwa wakilipwa Sh869,960 kila mwezi kwa jumla huku mtu mmoja ambaye ni mfungwa gerezani alikuwa akipokea mshahara wa Sh27,405 kila mwezi.

Ripoti hiyo pia ilifichua kuwa watu wanane ambao stakabadhi zao zilikuwa ghushi walikuwa wakipokea Sh318,500 kila mwezi huku watu 96 wanaopaswa wawe wamestaafu wakipokea Sh3.5 milioni kila mwezi.

Kulikuwa pia na watu 856 ambao walikuwa wakilipwa jumla ya Sh2.03 milioni za marupurupu kila mwezi.

“Bado hatujui watu 267 walikuwa wapi tukifanya uchunguzi huu muhimu kwa hivyo serikali ya kaunti inaweza tu kuamua kwamba wao ni wafanyakazi hewa ambao lazima wachukuliwe hatua zipasazo,” sehemu ya ripoti hiyo ikasema.

Ilibainika wafanyakazi 31 walikuwa na barua za ajira zilizotiliwa shaka uhalali wao, na wengine walikuwa hawafahamiki na wasimamizi wa idara zao.

Kwenye hotuba yake, Bw Obado alisema jumla ya wafanyakazi 2,615 kati ya 3,345 walipatikana kuwa wafanyakazi halali katika shughuli hiyo iliyolenga kung’oa wafanyakazi hewa waliokuwa wakipokea mishahara kiharamu.

Gavana huyo aliongeza kuwa ilitambulika kuna kasoro katika ulipaji marupurupu na kupandisha watu vyeo, hali ambayo husababishia kaunti hasara kubwa.