HabariSiasa

Miguna amrushia Raila makombora makali zaidi

May 22nd, 2018 3 min read

Na WAANDISHI WETU

WAKILI Miguna Miguna Jumatatu aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga akimtaja kama “mnafiki” ambaye amemezwa na utawala wa Jubilee.

Bw Miguna alitaja kuwa kinaya kwa Bw Odinga kujitakasa mbele ya Wakenya, ilhali ndiye kiini kikuu cha masaibu yanayomkumba kuhusu paspoti yake.

Kwenye ujumbe alioweka mtandaoni kutoka Canada jana, Bw Miguna alisema amemfanyia kazi Bw Odinga kwa muda mrefu na hivyo anafahamu bayana kwamba ana uraia halisi wa Kenya.

“Nimemfanyia kazi Bw Odinga kwa kushikilia nyadhifa mbalimbali tangu niliporejea Kenya. Ningefanya haya bila Bw Odinga kufahamu kwamba mimi si raia wa Kenya?” akashangaa Bw Miguna.

Wakili huyo alionyesha kukasisirishwa na msimamo wa Bw Odinga kuhusu suala lake la kurejeshewa paspoti yake ya Kenya akimtaja kigogo huyo wa upinzani kama asiye na msimamo imara.

“Wakati Raila alipoenda kortini kulalamikia matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2017, alisisitiza kila mtu aheshimu uamuzi wa mahakama. Imekuwaje sasa Raila huyo huyo hataki maafisa wa serikali kuheshimu maagizo 13 ya mahakama kuhusu suala la paspoti yangu,” alishangaa Bw Miguna.

Wakili huyo amekuwa akimshambulia Bw Odinga kwa siku kadhaa sasa kufuatia matamshi ya kiongozi wa ODM kuwa wakili huyo aliyemwapisha kuwa “rais wa wananchi” mnamo Januari 31 anafaa tu kujaza fomu ya kuomba uraia wa Kenya.

Hapo Jumatatu, Bw Miguna, ambaye wiki jana aliteuliwa na Gavana Mike Sonko wa Nairobi kuwa naibu wake, alisisitiza yeye ni raia wa Kenya kikatiba na akashangaa ilikuwaje akaanza kuambiwa si Mkenya licha ya kukubaliwa kupiga kura tangu 2002: “Nilipiga kura 2002, 2007 na 2017. Pia niligombea ugavana wa Nairobi.

Nilipewa vyeti na idara husika kabla ya kuwania ugavana. Pia nimekuwa nikilipa ushuru kama Mkenya. Sina rekodi yoyote ya uhalifu tangu nizaliwe.”

 

Raila alitumia paspoti za Uganda na TZ

Aliendelea: “Raila alipotoroka Kenya alitumia paspoti ya Uganda. Alipoenda Ujerumani Mashariki alitumia ya Tanzania. Kwani mimi si binadamu kama wengine?”

“Sijatoka familia kubwa. Huenda sikurithi chochote. Lakini nina akili timamu na sitakubali yeyote kuninyima haki zangu za kibinadamu na nitaendelea kutetea utawala wa haki,” akasema.

Alidai kuwa nia ya kumtaka kuomba upya uraia wa Kenya ni kumzuia kugombea cheo kikubwa 2022 kwa sababu Katiba inataka mgombeaji awe na uraia wa Kenya kwa miaka 10 au zaidi, ambayo hatakuwa amefikisha akipewa uraia sasa.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa chama cha Wiper, ambaye pia ni Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana, amesema mwafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga hautafaidi upinzani bali Bw Odinga peke yake.

Bw Kibwana pia amemshauri kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka kusahau mkataba aliofanya na Bw Odinga 2017.

“Tungependa kumuuliza Bw Kalonzo kwamba kuanzia sasa, asiwe na yeyote wa kushauriana kwa niaba yake. Kusalimiana kunaweza tu kuwa kati ya watu wawili.

Kusalimiana kwa Raila ni kwake yeye tu. Nasema haya nikiwa na heshima kubwa kwa Raila. Lakini sasa Kalonzo lazima aunde mwelekeo wake wa kisiasa baada ya 2017,” Prof Kibwana alisema.

 

Muungano bila Raila 

Katika taarifa yake ambapo anatazama hali ya kisiasa nchini siku zijazo kufuatia mkataba baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, Profesa Kibwana anasema kuwa upinzani unastahili kuungana na kuwa dhabiti hata bila Bw Odinga.

Raila alijitenga na vinara wenza katika muungano wa NASA na kuzungumza na Rais Kenyatta ambapo waliafikiana kushirikiana.

Lakini Bw Odinga amekuwa akidai NASA ingali imara japo wadadisi wanasema muungano huo ulisambaratika.

Profesa Kibwana ambaye alisaidia kuunda mkataba kati ya Bw Musyoka na Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, alitoa maoni yake kuhusiana na hatima ya muungano wa upinzani hasa kufuatia uhusiano wa Bw Odinga na chama tawala cha Jubilee.

Iliaminika kuwa sehemu ya mkataba, ambao pia ulishuhudiwa na msomi Profesa Makau Mutua, Bw Odinga anafaa kuunga mkono azima ya Bw Kalonzo ya kuwania urais 2022.

“Tunashukuru kuwa salamu za kwanza zilibadilisha mazingira ya kisiasa ya Kenya. Kilikuwa kitendo cha ujasiri na uzalendo. Lakini maoni yangu ni kuwa Bw Kalonzo, Mudavadi na Wetang’ula lazima waunde maisha yao wenyewe ya kisiasa bila kuhusisha yaliyojiri 2017. Kipindi hicho sasa kimefungwa,” alisema Bw Kibwana.

Kulingana na gavana huyo, Bw Musyoka lazima afanye miungano na makundi mengine ya wapigaji kura nchini na kuanzisha mazungumzo na Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na viongozi wengine wote wa kitaifa.”

“Wacha afanye salamu na hata kuzua ‘misukosuko ya moyo’ ambayo itatufaidi sisi na Kenya,” alisema Bw Kibwana.

Aliongeza: “Ni uamuzi wa Mhe Raila Odinga kuamua wakati ukifika ikiwa atalipa deni lake la kisiasa kwa wenzake wa NASA 2017. Lau sivyo, lazima tuwe tayari kupata ushindi bila kuhisi vibaya.”

Wiki mbili zilizopita Wiper kilimpatia Bw Musyoka idhini ya kuzungumza na vyama vingine kwa lengo la kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Musyoka amekuwa akisema kwamba atakutana na viongozi tofauti kwa lengo la kuunganisha Wakenya.

Ripoti ya WANDERI KAMAU, PIUS MAUNDU Na BENSON MATHEKA