Miguna awajibu watumiaji mitandao ya kijamii kuhusu mwonekano wake wa ‘kukonda’

Miguna awajibu watumiaji mitandao ya kijamii kuhusu mwonekano wake wa ‘kukonda’

Na MARY WANGARI

MWANASIASA aliyefurushwa nchini Miguna Miguna amefungua moyo kufuatia hisia za baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhusu hali yake ya kiafya.

Wakili huyo anayefahamika kwa ujasiri wa kueleza hisia zake, alijitokeza kuwakabili wanamitandao wadadisi kufuatia picha aliyochapisha mnamo Ijumaa, Julai 13, 2020, ambapo alionekana kubadilika pakubwa.

Ili kuwaondolea shaka wafuasi na wakosoaji wake mitandaoni, Bw Miguna aliamua kufafanua sababu zake za kupunguza uzani na mvi kujitokeza, akisema ilikuwa ishara ya afya njema na jambo la kawaida katika umri wake.

“Kupunguza uzani ni vyema kiafya. Unene mnaochukulia kuwa ishara za ufanisi ni dalili za kifo kinachojongea kutokana na maradhi ya shinikizo la damu, kisukari na mengineyo,”alihoji Bw Miguna kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Aidha, aliwapuuzilia mbali washindani wake kisiasa akidai wao hupaka rangi nywele zao ili kuficha mvi kwa sababu ya kukosa kujithamini.

“Mwanamme yeyote mwenye umri wa zaidi ya miaka 40 ana mvi. Waporaji wenu hupaka rangi mvi na ndevu zao kutokana na kutothamini nafsi zao,” alisema.

Yote hayo yalianza baada ya mwanaharakati huyo kuchapisha kwenye Twitter, picha yake akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Afrispain, mnamo Ijumaa, Julai 10, 2020.

Katika picha hiyo, Bw Miguna, anayefahamika kwa kimo chake kirefu na umbo lake nene, alikuwa amevalia shati la samawati na kaptura nyeusi, na alionekana kupunguza uzani pakubwa huku mvi zikijitokeza kidevuni mwake.

“Nilikutana na Bw Jackson Igbinosun katika Black Gold Think Tank usiku wa jana jijini Toronto. Ndevu za chumvi na pilipili zinajitokeza vyema,”Bw Miguna alinukuu picha yake.

Hata hivyo, wanamitandao hawakuchelewa kugundua mabadiliko hayo kwenye maumbile ya yake na wakafurika upesi kwenye ukurasa wake kuelezea hisia zao.

Baadhi hawakuchelea kumweleza wazi mwanasiasa huyo anayefahamika kama ‘jenerali’ miongoni mwa wafuasi wake, kwamba alikuwa amebadilika sana.

“Jenerali unaonekana umekonda,” alisema Shady Magero

“Yaonekana umerejea na kichwa kilichojaa mvi jenerali?”

“Wewe si jenerali niliyekuwa nikimjua,” alieleza Ibrahim Adow

Baadhi ya wafuasi wake walielezea wasiwasi wao kwamba Bw Miguna angekosa nguvu za kuendelea kupigania mageuzi huku wengine wakimtahadharisha kuhusu athari ya kupunguza uzani.

Na jenerali umekonda? Utaweza kutuongoza hadi katika nchi ya ahadi kweli?” alisaili Yoh Bruh.

“Miguna unapoteza uzani haraka sana. Bila shaka unafanya mazoezi wakati huu wa janga. Kumbuka mwanamme aliyekonda hatiliwi maanani nchini Kenya,” alishauri Lamborghini A.

Kuna walitoania kuwa wakili huyo alikuwa akifanya mazoezi ya kujiandaa kurejea nchini kwa kishindo.

Bw Miguna ambaye ni mkosoaji sugu wa serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na handisheki kati ya Kiongozi wa Taifa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, alitimuliwa nchini 2018, baada ya kuongoza uapishaji wa Bw Odinga kama “rais wa umma.”

Kwa sasa wakili huyo ametafuta hifadhi Canada baada ya juhudi zake za kurejea nchini kugonga mwamba mara mbili.

You can share this post!

Manchester City waponea adhabu baada ya CAS kubatilisha...

Kazi ya uchoraji yamwezesha kupata hela kipindi hiki cha...

adminleo