Habari MsetoSiasa

Miguna: Korti yaita Kihara afafanue ukaidi wa serikali

January 11th, 2020 2 min read

Na Richard Munguti

MWANASHERIA Mkuu Paul Kihara ameagizwa afike mahakamani Jumatatu kueleza kwa nini Serikali haijafanikisha kurudi kwa wakili na mwanaharakati Dkt Miguna Miguna kama ilivyoagizwa na korti.

Dkt Miguna yuko jijini Berlin Ujerumani anakosubiri Serikali itekeleze agizo la mahakama kuu kuhusu kurejea kwake.

“Wakenya wenzangu mnaotaka kujua hali yangu, nataka kuwaarifu kuwa ni mzima kama kigongo. Niko jijini Berlin, Ujerumani nikisubiri maafisa wakuu serikalini watii agizo la mahakama kufanikisha kurejea kwangu Kenya,” Dkt Miguna alisema katika mtandao wake wa Twitter.

Katika mahakama kuu jana, Jaji John Mativo alimwamuru Bw Kihara afike kortini kueleza sababu ya kutotii agizo la mahakama.

Ombi la aidha Bw Kihara ama wakili mkuu wa serikali Kennedy Ogetto afike kortini lilitolewa kutokana na ombi la wakili wa mwanaharakati huyo Dkt John Khaminwa.

“Ni Bw Kihara ama wakili mkuu wa Serikali Bw Kennedy Ogetto wanaoweza kueleza hii mahakama kwa nini maagizo yake hayatekelezwi,” alisema Dkt Khaminwa.

Wakili huyo alisema tangu 2018 maagizo ya korti kumhusu Dkt Miguna yamepuuzwa.

Jaji Mativo alitahadharisha kwamba mahakama haitachukulia kwa mzaha madai kuwa maagizo yake yanapuuzwa.

“Wakati umewadia hii mahakama itumie mamlaka na nguvu iliyopewa na Katiba,” alisema Jaji Mativo.

Jaji huyo alisema suala la Dkt Miguna kurudi nchini linapasa kutatuliwa kabisa.

“Licha ya kupokea maagizo ya kufanikisha kurudi kwa Dkt Miguna nchini, maafisa wakuu wa Serikali wameyakaidi kwa madharau,” alisema Dkt Khaminwa.

Dkt Miguna alifurushwa nchini Kenya 2018 baada ya kumwapisha kinara wa upinzani Raila Odinga kuwa “ rais wa wananchi.”

Lakini wakili wa Serikali alikariri kuwa Serikali haipingi kurudi kwa Dkt Miguna.

Mahakama ilielezwa kwamba Dkt Miguna anatakiwa kuenda katika afisi ya Ubalozi wa Kenya, ng’ambo kupewa pasipoti ya kutumia kurejea nchini.

Mahakama ilielezwa kwamba Serikali bado haijafutilia mbali arifa kumhusu Dkt Miguna kwa mashirika ya ndege za kimataifa kwamba yasimruhusu aabiri ndege zao.

Agizo hilo la jana linajiri baada ya uamuzi uliotolewa wiki iliyopita na Jaji Weldon Korir kwamba Serikali ifanikishe kurudi nchini kwa mwanaharakati huyo.