Habari Mseto

Miguna kujulikana kama atateuliwa naibu gavana wiki hii

June 12th, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

HATIMA ya uteuzi wa mwanaharakati wa upinzani Miguna Miguna kuwa naibu gavana wa Kaunti ya Nairobi inatarajiwa kujulikana wiki hii wakati mswada kuhusu uteuzi huo utawasilishwa kwa bunge la kaunti.

Spika wa bunge hilo, Bi Beatrice Elachi, Jumatatu alisema uteuzi huo uliofanywa na Gavana Mike Sonko utashughulikiwa inavyohitajika kisheria hata kama Dkt Miguna hayuko nchini.

“Tutawasilisha mswada wa uteuzi huo katika bunge la kaunti juma hili. Singependa kuzungumzia suala hili kwa mapana kwa sababu ni suala linalohitajika kujadiliwa mbele ya bunge la kaunti,” akasema Bi Elachi jana alipohojiwa kwenye runinga ya Citizen.

Dkt Miguna, ambaye alidai hakufahamishwa rasmi kuhusu uteuzi wake lakini hajafafanua kama atakubali uteuzi huo au la, alitimuliwa nchini na serikali kwa madai kwamba si raia wa Kenya baada ya kumwapisha Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’.

Uteuzi wake kuwa naibu gavana wa jiji kuu la Kenya mwezi uliopita uliibua utata hasa katika Chama cha Jubilee kwani viongozi wengi wa chama hicho walilalamika kuwa lazima naibu gavana awe ni mwanachama wa Jubilee na akubalike kwa wanachama na kwa viongozi wakuu wa chama.

Hata hivyo, baadaye viongozi mbalimbali chamani hasa madiwani walisema gavana huyo ana haki kumteua mtu yeyote anayetaka kuwa naibu wake kwani ameruhusiwa kisheria.

Bw Sonko alitetea hatua yake na kusema anaamini Dkt Miguna ndiye ana uwezo wa kukabiliana na matapeli anaodai wanamhangaisha anapojaribu kufanya mabadiliko ya kuboresha jiji.

Bi Elachi jana alisema mwelekeo halisi kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa uteuzi huo utabainika wiki hii.

“Wakati uteuzi utakapowasilishwa kwa bunge la kaunti wiki hii, mswada utaendelea mbele kama inavyohitajika katika sheria za bungeni,” akasema.