Habari MsetoMakalaSiasa

Miguna Miguna: Nilivyokula samaki 'kwa macho' katika kituo cha polisi

February 12th, 2018 3 min read

Wakili mbishi aliyefurushwa humu nchini Dkt Miguna Miguna. Ameapa kurudi Kenya ‘haraka iwezekanavyo’. Picha/ Maktaba

Na LEONARD ONYANGO

Kwa Muhtasari:

 • Dkt Miguna asema aliletewa ugali, samaki na mboga lakini akalazimishwa kuingia katika gari la polisi kabla ya kuanza kula
 • Alizuiliwa kwa zaidi ya siku tano katika vituo mbalimbali vya polisi
 • “Nilisikia polisi niliokuwa nao ndani ya gari wakijigamba namna walivyofanikiwa kuwachezea shere wanahabari”
 • Aliketi ndani ya gari kwa zaidi ya saa tano na baadaye polisi walitokea na tiketi ya ndege na stakabadhi zilizoonyesha alikuwa mhamiaji haramu

MWANAHARAKATI wa NASA Miguna Miguna amevunja ukimya kuhusu mateso aliyopitia mikononi mwa polisi huku akielezea alivyokula samaki ‘kwa macho’ katika Kituo cha Polisi cha Inland Container Depot, Barabara ya Mombasa, Nairobi.

Kupitia mtandao wa Facebook, Dkt Miguna alisema aliletewa ugali, samaki na mboga ya kienyeji kwa ajili ya chakula cha jioni lakini akalazimishwa kuingia katika gari la polisi na kuelekea katika uwanja wa ndege wa JKIA kabla ya kuanza kula.

“Nilipokuwa nakijiandaa kula mlo wa samaki, ugali na mboga za kienyeji nilioletewa na msimamizi wa kituo (OCS) muungwana, maafisa wa polisi wakatili walijitokeza na kuniambia “tunaondoka sasa”. Huo ndio ulikuwa mlo wangu wa siku lakini niliacha na kuondoka,”| akasema Dkt Miguna.

 

Siku tano ndani

Dkt Miguna aliyekamatwa mnamo Februari 2, kwa kumwapisha kinara wa NASA Raila Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’, alizuiliwa kwa zaidi ya siku tano katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Nairobi na Kaunti ya Kiambu kabla ya kusafirishwa nchini Canada kutokana na kigezo kwamba si Mkenya.

“Nilipoingia ndani ya gari, dereva aliendesha kwa kasi  kutoka katika Kituo cha Polisi cha Inland Container Depot na dakika 25 baadaye tulikuwa katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA),” akasema.

Dkt Miguna alikuwa amezuiliwa katika kituo cha polisi Inland Container Depot kabla ya kupelekwa katika Mahakama ya Kajiado kufunguliwa mashtaka ya kushiriki katika uhaini.

Baada ya kusomewa mashtaka katika mahakama ya Kajiado alirejeshwa tena katika kituo hicho huku kinara wa NASA Raila Odinga na wafuasi wake wakimngojea katika Mahakama ya Milimani Nairobi hadi saa tatu usiku.

Mara baada ya kukamatwa, Dkt Miguna alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Githunguri  na baadaye akahamishiwa kwenye kituo cha Lari katika Kaunti ya Kiambu.

Huu ndio msururu wa matukio kwa mujibu wa Dkt Miguna:

 • Februari 2 saa 5a.m, maafisa 35 wa polisi wavamia nyumbani kwa Miguna na kulipua lango kuu na mlango wa choo kwa kilipuzi.
 • Polisi wanampokonya Miguna simu na kutishia kumfunga macho kwa kitambaa na kisha kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Githunguri
 • Saa 5pm mawakili wake Edwin Sifuna, Waikwa Wanyoike na Willis Otieno wanaenda katika Kituo cha Polisi cha Githunguri
 • Usiku wa manane  polisi wakamtoa Bw Miguna katika Kituo cha Githunguri na kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Lari. “Kituoni Lari nilisimama seli kwa muda wa saa 24 bila kulala wala kuketi”

 

 • Februari 5 mchana: Polisi wanawasili na kumuagiza kuingia ndani ya gari. Magari matatu yanawafuata. Polisi wanafanikiwa kuwachanganya wanahabari na wafuasi wa NASA ambao walifuatilia gari tofauti. “Nilisikia polisi niliokuwa nao ndani ya gari wakijigamba namna walivyofanikiwa kuwachezea shere wanahabari.
 • Gari alilokuwemo Miguna linafululiza hadi katika Kituo cha Depot Police katika eneo la Embakasi Mashariki. “Kituoni hapa kwa mara ya kwanza napewa chakula kizuri, maji safi ya kuoga, mswaki na blanketi mbili zilizochakaa”.

 

 • Februari 6 asubuhi: maafisa wa polisi 15 wenye miraba minne wanawasili na kumwagiza  kuingia kwenye gari waliendesha gari hadi katika kituo cha mafuta katika eneo la Athi River na baadaye wakaendesha kwa kasi katika Barabara ya Kajiado.
 • Hatimaye alijipata katika mahakama ya Kajiado.
 • Nilipelekwa mbele ya hakimu ambaye aliagiza nipelekwe katika Mahakama ya Milimani Nairobi kabla ya saa tisa unusu mchana.
 • Badala ya kumpeleka katika Mahakama ya Milimani, polisi walimrejesha katika kituo cha Container Depot.
 • Hata hivyo, walipofika kituoni walimfungia ndani ya gari kwa takribani saa tano na kumpokonya paspoti yake ya Kenya.
 • Baadaye walimtoa nje ya gari na kumtaka kwenda kando kuzungumza. Kabla ya kuzungumza aliomba ruhusa ya kwenda chooni. “Walikubali niende chooni ila wakanipa maafisa watano wa kunisindikiza”.
 • Alipotoka chooni alizungukwa na maafisa 10 ambao walianza kumpekua mifukoni ambapo walipata paspoti yake ya Canada.
 • Takribani saa moja baadaye, aliletewa mlo lakini kabla ya kuanza kula, aliingizwa ndani ya gari na kupelekwa kwa kasi katika uwanja wa ndege wa JKIA.
 • Aliketi ndani ya gari kwa zaidi ya saa tano na baadaye polisi walitokea na tiketi ya ndege na kumkabidhi simu yake iliyokuwa imeharibika pamoja na stakabadhi zilizoonyesha kwamba alikuwa mhamiaji haramu asiyetakiwa.
 • Miguna asafiri kuelekea Canada.