HabariSiasa

Miguna Miguna sasa awaomba Wakenya wamchangie hela arudi nchini

March 7th, 2018 1 min read

Na WYCLIFFE MUIA

WAKILI Mbishi Miguna Miguna sasa anawaomba Wakenya wakarimu wamchangie pesa za nauli ya ndege ili aweze kurejea nchini kutoka Canada, kuendeleza kampeni za mageuzi ya uchaguzi.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Bw Miguna vilevile anaomba mchango wa pesa za kuwalipa mawakili waliomtetea mahakamani pamoja na pesa za kugharamia ukarabati wa nyuma yake.

“Nahitaji nauli ya kurudi nyumbani. Pia nahitaji pesa za kujenga upya nyumba yangu iliyoharibiwa. Mawakili wangu waliotetea uraia wangu kortini pia hawajalipwa tangu Februari. Unaweza kunichangia? Kuwa huru kufanya hivyo,” Bw Miguna aliandika katika akaunti yake ya Twitter.

Wakili huyo alitimuliwa nchini mnamo Februari 6 hadi Canada na serikali ya Kenya ikampokonya pasipoti yake baada ya kudaiwa kuwa nchini kinyume cha sheria.

Dkt Miguna aliwafokea waliomtaka atumie hela zake mwenyewe akisema wameleweshwa na wizi wa mali ya umma. Picha/ Twitter

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alisema Bw Miguna alijivua uraia wake wa Kenya miaka ya1980 na akapata uraia wa Canada.

Hata hivyo, mnamo Februari 16 Mahakama Kuu iliagiza serikali kumrejeshea wakili huyo vyeti vyake vya usafiri na kumpa nafasi ya kerejea Kenya.

Akitoa agizo hilo Jaji Chacha Mwita alisema Miguna yuko huru kutumia pasipoti ya Canada kurejea Kenya iwapo serikali itamnyima pasipoti ya Kenya.

Akiwahutubia wafuasi wa muungano wa NASA nchini Canada, Bw Miguna alisema anahitaji kurudi Kenya ili apambane na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.

Aliwataka Wakenya wanaoishi Canada waungane naye kushinikiza mageuzi ya uongozi nchini akisema kinara wa upinzani Raila Odinga anaendelea kuzeeka hivyo sharti watu warithi nafasi yake.

“Raila sasa ana miaka 73 na kwa sababu ni binadamu hataishi milele..atakufa tu. Ni lazima tujipange kuendeleza juhudi za ukombozi wa Kenya,” alisema Bw Miguna.