Habari MsetoSiasa

Miguna sasa amlaumu Raila kwa kushindwa kumnusuru

April 1st, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya kwanza kiongozi wa vuguvugu la NRM Miguna Miguna amemsuta kiongozi wa NASA Raila Odinga kwa kufeli kumsaidia kurejea nchini salama.

Katika taarifa aliyotuma Jumamosi kutoka uwanja wa ndege wa Dubai, Dkt Miguna alimkashifu Bw Odinga kwa kuendelea kushirikiana na watu aliodai kuwa ndio wanaodhulumu.

“Raila Odinga hawezi kuendelea kufurahia Sikukuu ya Pasaka nje ya nchi huku akiendelea kula pamoja na wadhalimu ilhali yule aliyemwapisha kama Rais wa Wananchi” anaendelea kudhulumiwa na watu hao hao walioiba kura zake na kuamuru mauaji ya kinyama ya wafuasi wake,” akasema.

Japo Bw Odinga hajatoa taarifa rasmi kuhusu masaibu yaliyomfika Bw Miguna tangu alipozuiwa kuingia nchini Jumatatu wiki jana, kiongozi huyo alifika katika uwanja wa ndege wa JKIA katika kile kilichosemekana kuwa jaribio la kumsaidia mwanaharakati huyo.

Hata hivyo, juhudi zake (Raila) ziligonga mwamba Miguna alipoendelea kuteswa katika uwanja huo na hatimaye akafurushwa hadi Dubai baada ya kuleweshwa na dawa za kupoteza fahamu.

Mnamo Alhamisi Bw Odinga pia alihudhuria kikao cha Mahakama ya Milimani kusikiliza kesi ya kupinga kufurushwa kwa Bw Miguna.

Hata hivyo, tofauti na hapo awali, kiongozi huyo wa ODM ambaye aliandamana na mfanyabiashara Jimi Wanjigi hakushabikiwa. Hii ni ishara kwamba wananchi hawakufurahishwa na kushindwa kwake kumnusuru Bw Miguna licha ya kuwepo muafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Miguna ambaye anasema anahitaji huduma za matibabu baada ya kudungwa dawa ya kumpoteza fahamu amewataka wafuasi wake kufanya maandamano kushinikiza arejeshwe Kenya, akisema hayuko tayari kuenda popote.

“Wadhalimu walioko mamlakani kinyume cha sheria walinidunga sindano ya sumu na kemikali nyingine za kusababisha magonjwa. Kwa hivyo, nahitaji huduma za matibabu kwa dharura,” akasema, ingawa inadaiwa kuwa amekuwa akipokea matibabu katika hospitali moja nchini Dubai.

“Nawaomba wafuasi wangu kuandaa maandamano kushinikiza nirejeshewe haki yaki yangu ya kuzaliwa na kikatiba…niruhusiwe kurejea nyumbani.

Watetezi wa haki za binadamu wapinge vitendo hivi vya ukiukaji wa haki zangu vinavyoendeshwa na Uhuru Kenyatta, William Ruto, Fred Matiang’i, Boinnet na Kihalangwa,” akasema.

Mnamo Ijumaa Wakenya walimshutumu vikali Bw Odinga kwa masaibu yaliyomkubwa Miguna kwa kipindi cha juma moja tangu alipojaribu kurejea nchini kutoka Canada.

Kwenye jumbe katika mitandao ya kijamii walimkashifu Odinga kwa kutofanya kumwokoa Miguna hata baada ya kutia saini mwafaka kati yake ni Rais Uhuru Kenyatta Machi 9.

“Kimya chako wakati Miguna Miguna anateswa ni usaliti mkubwa wa upinzani.Wafuasi wako wanateswa na hauwezi kuongea kwa sababu ulinyamazishwa kwa mabilioni ya fedha,’ aliandika Fred Omulo katika twitter.