Habari za Kitaifa

Mihadarati: Gavana Nassir atofautiana na Gachagua

February 28th, 2024 2 min read

NA VALENTINE OBARA

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, amekosoa msimamo wa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu kujitolea kwa kaunti kukabiliana na ulanguzi na matumizi ya dawa za kulevya katika eneo la Pwani.

Mnamo Jumatatu alipokuwa akihutubia kongamano linalohusu pombe haramu na utumizi wa dawa za kulevya eneo la Pwani, Bw Gachagua aliwakashifu viongozi wa ukanda huo kwa kukosa kuzuia ipasavyo kuenea na matumizi ya pombe haramu na dawa za kulevya.

Naibu Rais aliwakashifu vikali viongozi waliokwepa hafla hiyo, akihoji kujitolea kwao kupambana na janga la dawa za kulevya linaloathiri vijana wengi katika eneo hilo.

“Kwa nini viongozi wa Pwani wako kimya huku vijana wetu wakiuawa na kuharibiwa na dawa za kulevya? Mbona wengine hawapo, huu ni mkutano muhimu sana wa kujadili uwepo wa idadi ya watu wetu. Haya ni mazungumzo ambayo kila kiongozi aliyechaguliwa anafaa kuwa sehemu yake kwa sababu ni tatizo kubwa,” akasema.

Miongoni mwa viongozi ambao hawakuhudhuria hafla hiyo ni Bw Nassir ambaye badala yake aliwakilishwa na naibu wake, Bw Francis Thoya.

Bw Nassir, ambaye alikuwa mbele ya wanachama wa Kamati ya Seneti jijini Nairobi wakati huo, baadaye alitoa taarifa akiitaka Serikali ya Kitaifa kutekeleza majukumu yake katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Gavana huyo pia alionekana kukosoa matamshi ya Naibu Rais kwamba kaunti hazichangii vita dhidi ya utumizi wa dawa za kulevya na kusema kuwa utawala wake umetekeleza mipango mbalimbali ya kushughulikia tatizo hilo.

Kulingana na gavana huyo, kaunti ilikamilisha ujenzi wa vituo viwili vya kurekebisha tabia huko Marimani, eneo bunge la Kisauni kwa wanaume na Shika Adabu, eneo bunge la Likoni kwa wanawake na pia ililipa zaidi ya Sh60 milioni kwa Shirika la Kusambaza Dawa nchini (KEMSA) kwa usambazaji wa dawa na vifaa vya ziada ambavyo ni pamoja na Methadone inayotumiwa kudhibiti uraibu wa dawa za kulevya.

“Serikali ya Mombasa imejitolea kukabiliana na tishio la matumizi ya dawa za kulevya. Tunatoa wito kwa Serikali ya Kitaifa kuafikiana na juhudi zetu na kushughulikia tatizo la usambazaji wa mihadarati ambalo liko chini ya mamlaka ya asasi za usalama,” akasema.

Mwaka uliopita, viongozi hao wawili walizozana vikali baada ya Bw Gachagua kudai kuwa gavana hakutumia pesa alizokusudiwa kukabiliana na athari za mvua ya El-Nino.

Bw Gachagua amefanya ziara nyingi Mombasa ambapo mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, mara nyingi ndiye humtembeza sehemu tofauti.

Mbunge huyo ambaye ndiye pekee aliyechaguliwa kwa tiketi ya UDA Mombasa ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa gavana huyo na inaaminika analenga kuwania kiti cha ugavana mnamo 2027.

Wakati wa kongamano hilo, naibu rais alimsifu Bw Ali kuwa kiongozi pekee wa kisiasa kutoka Mombasa ambaye alikuwa amewasiliana na Serikali ya Kitaifa kukabiliana na ulanguzi wa dawa za kulevya katika eneo hilo.

Wawili hao baadaye walihudhuria hafla katika eneo bunge la Nyali ya kuzindua madarasa 12 mapya katika Shule ya Msingi ya Freretown, wakiandamana na Waziri wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu, mwenzake wa Uchumi wa Baharini, Bw Salim Mvurya, Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani miongoni mwa wengine.