Kimataifa

Mihadarati: Mkenya ahukumiwa kifungo cha maisha jela nchini Uchina

July 26th, 2019 2 min read

Na AGGREY MUTAMBO na MARY WANGARI

MKENYA mwenye umri wa miaka 44 amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani nchini Uchina baada ya kupatikana na kosa la ulanguzi wa mihadarati.

Simon Wambua Mbuvi huenda akaungulika gerezani kwa miaka yake yote ya uhai duniani baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha gramu 947 ya kokeni kwa kutumia tumbo lake nchini Uchina

Alizabwa hukumu hiyo ya kifungo cha maisha gerezani na Jaji Mkuu Hu Peng na majaji wenzake Wen Fangdao na Huang Jian katika mahakama ya Chinese Intermediate People’s Court, katika Manispaa ya Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, kwa mujibu wa ripoti.

Mbuvi ambaye ilikuwa mara yake ya kwanza kusafiri nje ya Kenya, alikuwa akifanya kazi ya kibarua shambani kabla ya kuamua kujaribu riziki katika taifa hilo la Bara Asia mwaka 2018.

Aidha, ilikuwa mara yake ya kwanza kupatikana na hatia kisheria lakini sasa anakabiliwa na jinamizi la kufungiwa maisha yake yote pamoja na Wakenya wengine 30 wanaohudumu vifungo katika magereza ya Uchina kutokana na makosa mbalimbali.

Kwa mujibu wa ripoti, masaibu ya Mbuvi yalianza mwaka uliopita alipokutana na mwanamke aliyetambulishwa kama Brenda aliyemjia na kazi aliyotaka amfanyie kwa ahadi ya kumpa Sh211,150 kama mshahara wake

Brenda ambaye pia anafahamika kama Fridah alishughulikia mambo yote ikiwemo kumnunulia Mbuvi tiketi, kumlipia ada ya cheti cha usafiri na hata kumuunganisha na watu wengine bila kumfichulia kwamba kazi aliyotarajiwa kufanya ilihusu ulanguzi wa mihadarati.

Mbuvi alifunga safari mnamo Novemba 24 kupitia Addis Ababa ambapo alikutanishwa na wanaume wengine wawili kama wenyeji wake.

Walimlisha na baada ya kupumzika wakamshawishi kumeza tembe 79 kwa kutumia maji na soda. Kisha walimsindikiza kuabiri ndege kuelekea Uchina huku wakimpa onyo kali la kutokula chochote katika safari hiyo yote ya muda wa saa 12.

Alipotua katika taifa hilo la bara Asia alipitia kwenye malango ya ukaguzi yenye mitambo ya eksirei iliyoashiria “kuwepo kwa chembechembe za kutiliwa shaka.”

Ushahidi

Maafisa wa Idara ya Uhamiaji walimkabidhi Mbuvi mikononi mwa maafisa wa Idara ya Kukabiliana na Ulanguzi wa Bidhaa katika Uwanja wa Ndege wa Guangzhou Baiyun ambapo kulingana na ushahidi uliowasilishwa kortini, tumbo la Mbuvi lilikuwa limebeba chembechembe zisizo za kawaida.

Mkenya huyo alizuiliwa kwa muda wa siku mbili ambapo aliweza kutoa tembe hizo zote 79 zenye uzito wa gramu 947.03 na katika muda huo aliweza kurithisha mamlaka ya Uchina kwamba yeye binafsi hakuwa mtumiaji wa mihadarati.

Mahakama hiyo ilimpa Mbuvi muda wa siku 10 kukata rufaa akiendelea kuhudumu kifungo chake cha jela.

Kwa sasa Mkenya huyo anakabiliwa na uhalisia wa kutisha wa kusalia gerezani maisha yake yote ikizingatiwa mataifa ya Kenya na Uchina hayana mikataba ya kubadilishana wafungwa.

Cheti chake cha usafiri kitarejeshewa mamlaka ya Kenya.