KALUME KAZUNGU Na FARHIYA HUSSEIN
ZAIDI ya asilimia 60 ya wafungwa katika Kaunti ya Lamu ni vijana wa chini ya umri wa miaka 35, wengi wao wakihusishwa na ulanguzi na utumizi wa dawa za kulevya.
Haya ni kulingana na takwimu za idara ya mahakama eneo hilo.
Akizungumza kwenye gereza la Hindi jana Jumanne, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Lamu, Bw Allan Temba, aliwasihi vijana kujiepusha na ulanguzi wa dawa za kulevya.
Bw Temba alizungumza wakati alipoongoza kamati maalum ya maafisa wa idara ya mahakama, Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP), wawakilishi wa idara ya usalama na wanaharakati wa kundi la vijana la Kiunga Youth Bunge Initiative (KYBI), kuzuru jela ya Hindi kuhamasisha mahabusu kuhusiana na umuhimu wa kutii sheria za nchi.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba jamii inakosa viongozi wa kesho ambao ni vijana. Wengi wako jela. Ukitazama takwimu zetu utapata kati ya asilimia 60 na 70 ya wanaojipata jela ni vijana wa miaka 35 kwenda chini. Haya yote yanatokana na vijana hawa kujiingiza katika biashara ya kusafirisha, kutuma au kumiliki dawa za kulevya. Ni vyema tubadilishe tabia zetu na kuwa watu wema kwa nchi punde tunapokamilisha vifungo vyetu,” akasema Bw Temba.
Naibu Kamishna wa tarafa ya Amu, Bw Philip Oloo, pia aliwasihi vijana kujiepusha na mafunzo ya itikadi kali yanayosababisha ugaidi.
Bw Oloo alisema dawa za kulevya na ugaidi mara nyingi huambatana au kwenda sambamba, akitaja kuwa ni rahisi kwa watumiaji wa dawa za kulevya kujiunga na makundi haramu ya uhalifu.
“Twashukuru kwamba siku za hivi karibuni Lamu imeshuhudia idadi ndogo ya visa vya vijana kujiunga na makundi haramu. Tuzidi kuwa na nia moja ya kuweka amani nchini,” akasema Bw Oloo.
Kwa upande wake, Afisa wa KYBI, Bw Moses Maina, alisema shirika hilo litaendeleza juhudi za kuandaa warsha mbalimbali za kuhamasisha jamii na wafungwa kuhusiana na masuala yanayoathiri jamii.
Kaunti nyingi za Pwani huwa miongoni mwa zile zenye kiwango kikubwa cha matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana.
Wiki iliyopita, Rais William Ruto, aliagiza asasi husika za serikali kuziba mianya yote ambayo hufanikisha ulanguzi wa mihadarati hasa katika ukanda huo.
Katibu wa Mipango katika Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK), Sheikh Mohamed Khalifa, alitoa wito wa ushirikiano kati ya taasisi zote husika ili kusaidia kukomesha tatizo la dawa za kulevya.
“Tumeona watu waliopewa mamlaka ya kuzuia uuzaji wa dawa hizi haramu wakiishia kuwa wafanyabiashara wao wenyewe,” akadai Bw Khalifa.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Kenya (Supkem), Sheikh Muhdhar Khitamy, alisema watajitolea kushirikiana na serikali katika vita dhidi ya mihadarati eneo hilo.
Kulingana naye, kuna mbinu mpya ambazo zimefanya wanafunzi wengi kujitosa katika matumizi ya dawa za kulevya katika miaka ya hivi majuzi.
Subscribe our newsletter to stay updated