Kimataifa

Mihadarati yenye sumu inasambazwa Afrika, Ripoti

June 16th, 2024 2 min read

Na MASHIRIKA

ABUJA, NIGERIA

CHEMBECHEMBE za kemikali sumu zimegunduliwa kwa mara ya kwanza kuwa zinamezwa na watu wanaotumia mihadarati Barani Afrika, ripoti mpya imeonyesha.

Kemikali hizo hatari almaarufu kama Nitazenes, zimekuwa zikitumika kwa muda mrefu katika mataifa ya Magharibi na Barani Asia ambapo zimehusishwa na vifo vinavyotokana na matumizi ya kiwango cha juu.

Baadhi ya kemikali hizo zinaweza kuwa na nguvu ya hadi mara 100 zaidi kuliko heroni na mara kumi zaidi ya dawa za kulevya zinazofahamika kama fentanyl, kumaanisha kuwa watumiaji wanaweza kuathirika kutokana na kiwango kidogo tu na kuwaweka kwenye hatari ya kufa kutokana na madhara yake.

Ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano na shirika lisilo la kiserkali la Shirika la Mpango wa Ulimwengu Dhidi ya Uhalifu Uliopangwa Kimataifa, ililenga mataifa ya Sierra Leone na Guinea-Bissau.

Utafiti ulijumuisha vipimo vya mihadarati kwa jina kush, kemikali inayotokana na bangi na kisha kuchanganywa na dawa za kulevya kama vile fentanyl, tramadol na kemikali kwa jina formaldehyde.

Watafiti waligundua asilimia 83 ya chembechembe hizo nchini Sierra huku taifa la Guinea-Bissau likipatikana kuwa na asilimia 55.

“Shirika la Mpango wa Ulimwengu wa Kupambana na Uhalifu Uliopangwa Baina ya Mataifa (GI-TOC) linaamini kuwa matokeo haya ni ishara za mwanzo mwanzo kuwa nitazenes zimepenya katika soko la kuuzia dawa barani Afrika,” inaeleza ripoti hiyo.

Vijana wengi katika mataifa ya Afrika Magharibi na ya Kati wamegeuka waraibu wa mihadarati huku kati ya asilimia 5.2 na asilimia 13.5, wakitumia bangi, ambayo ndiyo mihadarati inayotumika zaidi katika bara hili, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Bio, mwaka huu alitangaza vita dhidi ya mihadarati inayofahamika kama kush ambayo inatumika zaidi nchini humo, akiitaja kama janga na tishio la kitaifa.

“Kemikali ya nitazenes zimegunduliwa mara kadhaa katika bidhaa zinazouziwa vijana katika eneo hilo na kuna uwezekano mkubwa watumiaji wanameza chembechembe hizo hatari bila kujua hatari inayowakodolea macho,” ilieleza ripoti hiyo.

Watafiti wamesema matokeo yao yanaashiria kuwa nitazenes zinaingizwa nchini Sierra Leone kutoka kwingineko na bidhaa inayouzwa kwa kutumia jina kush nchini Guinea-Bissau inajumuisha mchanganyiko wa kemikali ulio sawa na unaopatikana katika jiji kuu la Freetown.

“Maafisa katika mataifa hayo mawili ni sharti watoe vifaa vya kupima kemikali kama hatua ya kwanza kabisa katika kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya,” ilisema ripoti.

“Pasipo kufanya hivi, serikali za Sierra Leone, Guinea-Bissau na eneo lote kwa jumla hazitaweza kuangazia ipasavyo masoko ya mihadarati haramu katika mataifa haya na kubuni mikakati inayojikita kwenye ushahidi.”