Habari

Miili iliyofukuliwa Nanyuki ya mwanamke na wanawe wawili yafanyiwa upasuaji

November 20th, 2019 1 min read

Na JAMES MURIMI na NICHOLAS KOMU

SHUGHULI ya upasuaji wa maiti za marehemu Joyce Syombua na wanawe wawili imefanyika katika mochwari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nanyuki ambapo imebainika alipata majeraha ya silaha butu kichwani huku watoto wakinyongwa.

Familia ya mhanga wa mauaji ya unyama – Syombua – imeungana na wataalamu walioongozwa na mpasuaji mkuu wa serikali Dkt Johasen Oduor huku shughuli hiyo ikitarajiwa kuchukua muda takribani kutwa nzima.

Mamake Syombua – Maua Malombe – amejiunga na marafiki wawili wa familia katika mochwari.

Upande wa wapelelezi wa mauaji hayo uneongozwa na Mkuu wa Uchunguzi wa Jinai Laikipia Mashariki Jacob Muriithi.

Awali upasuaji uliratibiwa kufanyika Jumanne lakini shughuli hiyo ikaahirishwa hadi leo Jumatano.

Syombua alifariki akiwa na umri wa miaka 31, pamoja na wanawe Shanice Maua a;iyekuwa na umri wa miaka 10, na Prince Michael aliyekuwa na umri wa miaka mitano ambao miili yao ilipatikana imezikwa katika kaburi la kimo kifupi katika makaburi ya Nanyuki mjini.

Naibu Mkurugenzi wa Upande wa Mashtaka ya Umma eneo la Kati Peter Mailanyi aliambia mahakama ya Nanyuki mnamo Jumatatu kwamba muda zaidi ulihitajika maiti hizo kufanyiwa upasuaji.

Alisema sampuli za vinasaba zilikuwa zimechukuliwa tayari kuangaliwa na wataalamu kwa tathmini ya vipimo.

Peter Mwaura aliyekuwa na cheo cha Meja katika kambi ya Laikipia Air Base alifikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkuu Lucy Mutai.

Ndiye mshukiwa mkuu wa mauaji hayo.

Mshukiwa mwingine ni Collins Pamba.