Habari

Miili inayoaminika ni ya mwanamke na wanawe wawili waliotoweka kiajabu yapatikana

November 16th, 2019 2 min read

Na NICHOLAS KOMU na CHARLES WASONGA

MIILI mitatu inayoaminika kuwa ya mke wa mwanajeshi mmoja na wanawe wawili, waliotoweka majuma matatu yaliyopita, imepatikana imezikwa katika kaburi lenye kimo kifupi katika mtaa wa Thingithu, mjini Nanyuki ambapo imefukuliwa Jumamosi jioni.

Maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na polisi mmoja wa jeshi – Military Police – wamepata miili hiyo baada ya kuelekezwa mahala hapo na mwanajeshi huyo ambaye ni mshukiwa mkuu katika mauaji hayo.

Meja Peter Mwaura wa kambi ya wanajeshi wa Angani ya Nanyuki alikamatwa Alhamisi na polisi wa jeshi na kupokezwa kwa DCI.

Baada ya kuhojiwa kwa muda wa saa 24 katika kituo cha polisi cha Nanyuki na nyumbani kwake katika kambi hiyo ya kijeshi, mshukiwa huyo aliwaelekeza wapelelezi hadi katika eneo lililotengwa la makaburini katika mtaa wa Thingithu ulioko umbali wa kilomita moja kutoka kambi hiyo.

Huku akiwa amevalia tishati ya kijeshi, mwanajeshi huyo aliongoza kundi la maafisa wa DCI na KDF hadi pahala halisi ambapo miili hiyo ilizikwa.

Baada ya dakika 30 za uchunguzi na uchimbaji, polisi walipata magunia matatu yaliyosheheni miili hiyo mitatu iliyokuwa imeanza kuoza.

Gunia hilo lilifungwa kwa kamba ya plastiki na kuzikwa ndani ya kaburi hilo.

Wakati huo wote, mshukiwa aliketi ndani ya gari la maafisa wa DCI, akitazama miili hiyo ikitolewa na huku akificha uso wake usinaswe na kamera za wanahabari na wananchi waliofika hapo kufuatilia tukio hilo la kiajabu.

Hata hivyo, afisa wa upelelezi wa jinai Laikipia Peter Muinde amedinda kuthibitisha ikiwa miili iliyopatikana ni ya mwanamke aliyetoweka na wanawe wawili.

“Bado tunafanya uchunguzi wa kina kwa lengo la kutambua miili hiyo. Mtu fulani alituelekeza pahala ilipozikwa na tunajizatiti kuthibitisha ikiwa miili hiyo ni ya mwanamke huyo na wanawe wawili,” akasema Bw Muinde.

Bi Joyce Syombua, 31, na wanawe Shanice Maua, 10, na Prince Michael, 5, waliripotiwa kupota mnamo Okroba 27 baada ya kukaa kwa siku mbili nyumbani kwa Meja Mwaura. Waliwasili katika kambi ya Laikipia mnamo Oktoba 25 wakitoa mtaa wa Kayole, Nairobi

Bi Farizana Syombua, jamaa wa mwanamke huyo aliambia Taifa Leo kwamba alimtumia ujumbe mfupi kumuuliza ikiwa aliwasili Nanyuki na akajibu kwamba kila kitu kilikuwa shwari.

Syombua alimwarifu Bi Farizana, kwa njia ya ujumbe mfupi, kwamba Bw Mwaura alikuwa amewapeleka watoto kwa matembezi ndani ya kambi hiyo ya kijeshi.

Lakini Bw Mwaura alisema aliwaacha watoto hao na rafiki yake kwa sababu alitaka kufanya mazungumzo ya faragha na mkewe.

Mbele alikuwa amewaarifu polisi kwamba Syombua aliondoka kwenda Nairobi na watoto kwa matatu ya kampuni ya 4NTE Sacco.

Hata hivyo, watatu hao hawakufika nyumbani kwake Kayole, Nairobi hali iliyoibua hofu kuhusu usalama wao.

Awali, ripoti ilipelekwa katika vituo vya polisi vya Soweto na Nanyuki, na hivyo uchunguzi ukaanzishwa kuhusu kutoweka kwa watatu hao.

Simu

Kupatikana kwa simu yake ya mkononi ndani ya matatu moja ndiyo baadaye kulifichua siri ya kile kilichogeuka kuwa mauaji ya watatu hao na njama ya kufunika ukweli kuhusu kitendo hicho.

Baadaye polisi waligundua kuwa matatu ambapo simu hiyo ilipatikana haikusafiri hadi Nairobi.

Maafisa wa shirika linalosimamia matatu hiyo waliwaambia polisi kuwa ilikodiwa kwa shughuli ya kibinafsi katika eneo la Rift Valley mnamo Oktoba 28 na haikuenda Nairobi alivyodai Meja Mwaura.

Baadaye habari zilizotolewa na shahidi mmoja ndizo ziliwapa polisi mwelekeo ambao ulisaidia kutanzua kitendawili hicho.

Shahidi huyo aliambia polisi kwamba mwanajeshi huyo (Mwaura) alimtuma akanunue magunia matatu

Mwaura alikamatwa Alhamisi na Polisi wa Jeshi. Atawafikishwa mahakamani mnamo Jumatatu kujibu mashtaka ya mauaji kwa kukusudia.