Habari Mseto

Miili ya watatu waliouawa yapatikana imetupwa kijijini Rwera

November 1st, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Rwera, eneo la Murera, Juja wanaitaka serikali kuhakikisha usalama unaimarishwa.

Mnamo Jumatano asubuhi wiki hii miili mitatu ilipatikana imetupwa kwenye bwawa la maji na shamba la Kahawa.

Wakazi hao walisema wakazi wenzao waliokuwa wakienda kazini ndio waliitambua miili miwili ndani ya bwawa la maji na mwili mwingine katika shamba la Kahawa.

Wakazi hao walisema walidhania pengine miili hiyo ilitolewa mbali baada ya wahanga kuuawa na kutupwa maeneo hayo.

Walizidi kusema ya kwamba matukio kama hayo yamezidi kushuhudiwa katika siku za hivi karibuni huku wakazi wakihofia uhai wao.

Mkazi mmoja wa kijiji hicho cha Rwera, Bw David Waweru, alisema watu waliokuwa wakienda kazini ndio walipata miili hiyo ikielea kwenye bwawa moja eneo hilo.

“Jambo hilo lilitushtua kabisa ambapo tulipiga ripoti polisi na baadaye iliondolewa kwa uchunguzi zaidi,” alisema Bw Waweru.

Alisema tukio hilo limesababisha hofu kwa wakazi hao.

“Ifikapo saa moja za usiku hakuna yeyote anayeweza kutembea usiku kwa sababu kila mmoja huku anahisi anaweka hatarini uhai wake,” alisema Bw Waweru.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Bw Justine Mwangi ,alisema eneo hilo halina usalama na kwa hivyo serikali inastahili kuingilia kati.

“Kwa miezi kadha kuna watu fulani wamepatikana wakiwa wameuawa. Hata eneo hilo lina msitu mkubwa ajabu na kwa hivyo, ni vyema lishughulikiwe mara moja kabla watu wengi kuendelea kuuawa,” alisema Bw Mwangi.

Alisema kuna shamba la kahawa la Rwera na ifikapo jioni huwa kuna hatari unapotembea usiku.

Wakazi hao wanaitaka serikali ifanye hima kuona ya kwamba maafisa wa usalama wanapelekwa katika kijiji hicho ili wawe wakipiga doria majira ya usiku.

“Hayo mashamba ya kahawa ni hatari unapotembea peke yako kwa sababu za kiusalama. Unapokutana na wahalifu hakuna jinsi utakavyojinasua kutoka kwao ukiwa peke yako,” alisema Bw Mwangi.