Makala

Mikakati ya Dkt Ruto kudhibiti Jubilee

September 3rd, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA na GEOFFREY ANENE

NAIBU Rais William Ruto ameamua kudhibiti chama cha Jubilee kwa kuhakikisha ameshawishi maamuzi muhimu.

Haya yamebainika huku kukiwepo madai kwamba Dkt Ruto alisukuma Jubilee kudhamini mgombeaji katika uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra kama sehemu ya mikakati yake wa kukita usemi wake chamani na kufanikisha ndoto yake ya kuingia Ikulu mwaka 2022.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba uongozi wa chama awali haukutaka kudhamini mgombeaji Kibra ili usiathiri uhusiano mzuri uliopo kati ya kiongozi wake, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia handisheki.

Lakini chama hicho kililazimika kukubaliana na uamuzi wa Dkt Ruto ili kuzuia uwezekano wa viongozi wa Jubilee kuunga mkono wagombeaji tofauti katika uchaguzi huo wa Novemba 7 hali ambayo ingepanua zaidi ufa uliopo ndani ya chama tawala.

Mnamo Ijumaa wiki jana, mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEC), Andrew Musangi, alithibitisha kuwa mwanasoka McDonald Mariga, ambaye anapendelewa na Dkt Ruto, ni miongoni mwa watu 16 wangepigwa msasa ili katika harakati za kusaka anayehitimu kuwa mgombeaji wa Jubilee.

Kama ilivyodhihirika katika chaguzi ndogo za Wajir na Embakasi Kusini, Dkt Ruto anataka mgombeaji anayependelea ndiye aibuke mshindi katika uchaguzi mdogo wa Kibra ili kuimarisha nafasi yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hata hivyo, saa chache baada ya Jubilee kutangaza Mariga atapeperusha bendera ya chama, kiungo huyu aliyesakata soka yake katika mataifa ya Italia, Uhispania na Uswidi kati ya mwaka 2006 na 2018, amepuuzilia mbali madai hayo.

“Mimi si mradi wa mtu yeyote. Nawania kiti cha ubunge cha Kibra kwa sababu nataka ‘kurudisha mkono’ kwa jamii. Pia, nafahamu maisha ya watu wa eneo hili na kile wanachopitia,” akasema Mariga.

Enzi yake kama mchezaji, Mariga, 32, alichezea Enkopings SK na Helsingborg (Uswidi), Parma, Inter Milan na Latina Calcio (Italia) na Real Sociedad na Real Oviedo (Uhispania). Hajakuwa na klabu tangu Julai 1, 2018, hali ambayo pengine imemsukuma katika siasa kujaribu bahati yake.

Mariga alibwaga watu 15 kupata tiketi ya kupeperusha bendera ya Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Kibra utakaofanyika Novemba 7. Aliwabwaga Morris Kinyanjui, Walter Trenk, Ibrahim Said, Doreen Wasike, Oscar Kambona, Bukachi Chapia, Jane Githaiga, Jack Owino, Omondi Rajab, Daniel Adem, Daniel Orogo, Ramadhan Hussein, Fank Amollo, Timothy Kaimenyi na Geoffrey Mwangi.

Atapambana na mgombea wa ODM, ambaye atajulikana baada ya mchujo utakaofanyika Septemba 7, Eliud Owalo (Amani National Congress) na wagombeaji huru kadhaa.

Kiti hiki kiliachwa wazi baada ya Ken Okoth kuaga dunia Julai 26, 2019 jijini Nairobi baada ya kuugua kansa.

Duru kutoka ndani ya Jubilee zasema Dkt Ruto pia anapanga kudhibiti chama hicho kwa kuhakikisha kuwa wandani wake wanashinda viti vingi katika uchaguzi ambao utafanyika kuanzia Machi 2020. Uchaguzi huo utafanyika kutoka ngazi ya mashinani hadi kitaifa.

Itakumbukwa kuwa alitumia mbinu kama hii kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017, alipoingilia mchujo wa Jubilee na kuhakikisha kuwa wanasiasa wandani wake waliibuka washindi, hasa katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya.

Uchaguzi wa chama unapokaribia, wandani wa Dkt Ruto katika matawi ya Jubilee kote nchini sasa wanaamini wana idadi tosha ya wajumbe ambao wataweza kumuondoa Bw Raphael Tuju kutoka wadhifa wake wa Katibu Mkuu.

Dkt Ruto hafurahishwi na jinsi Bw Tuju anaendesha shughuli za chama hicho na Agosti alimtaja kama Katibu Mkuu wa chama tawala ambaye amepoteza mwelekeo na kugeuka mpanga mikakati wa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga.

“Kwa sababu ameonekana kuunga mkono Raila Odinga, tunahisi kuwa Bw Tuju anafaa kuiga mfano wa Bw David Murathe na kujiuzulu mapema. Asipofanya hivyo, tutahakikisha ameong’olewa mamlakani katika uchaguzi wa chama mwaka 2020,” mbunge wa Belgut Nelson Koech alisema juzi.

Hofu

Dkt Ruto anahofia kwamba wanaopinga azma yake kama Bw Murathe wanaweza kusambaratisha chama anachoamini ni maarufu miongoni mwa Wakenya.

Lakini ieleweke kwamba licha ya kutangaza kujiuzulu, jina la David Murathe bado liko katika orodha ya maafisa wa Jubilee, ambapo anaorodheshwa kama Naibu Mwenyekiti.

Inasemekana kuwa Rais Kenyatta alipinga nia yake ya kujiuzulu.

Yapo madai kwamba wafuasi wa Dkt Ruto pia wanapanga kumiliki jina la Jubilee kwa kuunda chama kipya cha Jubilee Republican Party ambacho atakitumia katika safari yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hii ni baada ya kubainika kuwa viongozi wa Jubilee wanaounga mkono handisheki wanapanga kukihama kubuni muungano mpya wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 na kukatiza uhusiano kati yao na Dkt Ruto.

Juzi Mbunge Maalum Maina Kamanda alifichua muungano huo utashirikisha chama cha ODM pamoja na “vyama vingine vyenye sera sawa na zetu”.