Habari za Kitaifa

Mikakati ya Gachagua haizai matunda, wakulima wa kahawa walia


MIKAKATI ya Naibu Rais Rigathi Gachagua ya kufufua sekta ya Kahawa inaonekana kugonga mwamba, huku wakulima waliokata tamaa wakionya kwamba kuendelea kupuuza zao hilo kutaathiri wakazi wa eneo hilo.

Katika kaunti za Nyeri, Kirinyaga na Murang’a, zinazoongoza kwa kilimo cha kahawa hasa wakulima wadogo, wakulima wamekuwa wakiandamana wakielezea kutamaushwa na kupungua kwa malipo ya zao hilo.

Wengine wanalalamikia kucheleweshwa kwa malipo na makato wanayosema ni wizi wa moja kwa moja wa mapato yao.

Matukio ya hivi majuzi katika eneo lote ni ishara tosha ya masaibu wanayopitia wakulima, kuonyesha kwamba mageuzi bado hayajafaulu kwani mambo yameanza kuharibika kwa zao hili ambalo ni tegemeo kuu la uchumi wa wakazi.

Kufufuliwa kwa sekta ya kahawa kulikuwa ahadi kuu ya kampeni ya Rais William Ruto na punde tu baada ya kuingia mamlakani, alimpa Naibu wake Rigathi Gachagua jukumu la kuongoza na kusimamia mageuzi katika sekta ya kahawa, chai na maziwa.

Mnamo Juni 10, 2024, serikali ilitangaza kuwa deni la Sh6.8 bilioni lililodaiwa vyama vya kahawa lingeondolewa lakini mchakato huo bado haujaanza.

Akihutubia wakulima wa kahawa huko Maragua, Kaunti ya Murang’a mapema Agosti, Bw Gachagua alisema serikali haitalegea katika mageuzi yanayoendelea katika sekta hiyo na kwamba mengi yatafanywa ili kuongeza mapato katika sekta ya kahawa huku serikali ikifuta madeni.

“Niliagizwa na Rais William Ruto kuongoza mageuzi na tunafanya vyema. Tumepiga hatua na kuwashinda mabroka na mapato ya mauzo ya nje yameongezeka maradufu katika mwaka mmoja uliopita,” alisema

Hata hivyo, katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, wakulima katika kanda nzima wamekuwa wakiandamana kwa kutamaushwa na maafisa wa vyama vya ushirika na mabroka ambao wanadai wanawapora.

Wakulima hao hawaonekani kukubaliana kabisa na kauli ya naibu rais na wameingia mitaani wakipinga kuendelea kufyozwa jasho lao.

Wiki iliyopita katika eneo la Mathira, anakotoka Bw Gachagua, wakulima kutoka vyama tofauti vya kahawa waliingia barabarani kuandamana kuelezea kutofurahishwa kwao na hali inayozidi kuwa mbaya.

Wakulima zaidi ya 5,000, wanachama wa chama cha wakulima wa Kahawa cha Baricho, walifunga barabara ya Karatina- Nairobi wakilalamikia malipo duni ya zao hilo pamoja na makato ‘yasiyoelezeka’ ya mapato ya msimu uliopita.

Wakulima walisema licha ya viongozi kuwaahidi bei ya chini ya uhakika ya Sh100 kwa kilo moja ya kahawa iliyowasilishwa kwa viwanda wakati wakati wa kampeni, hawajaona mabadiliko yoyote.

Baadhi walilalamika kuwa bado hawajapokea malipo yoyote licha ya kuhakikishiwa mara kadhaa na wasimamizi wa viwanda.

Katika kiwanda jirani cha Ndaroini, Mathira, hali ilikuwa hiyo hiyo wakulima walipofunga barabara wakilalamikia kupokea Sh60 kwa kilo ilhali walikuwa wakitarajia zaidi ya Sh100 kwa kilo kutoka kwa kampuni ya kibinafsi ya uuzaji kahawa ambayo walitia mkataba kuuza zao lao chini ya mfumo wa mauzo ya moja kwa moja.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, wakulima wanakumbwa na hali sawa.

Mnamo Julai 7, wakulima wa kahawa waliokuwa na hasira kutoka viwanda vya Kibirigwi na Ngugi-ini katika Kaunti Ndogo ya Ndia, waliingia barabarani kuandamana kulalamikia malipo duni.

Seneta wa Kirinyaga James Murango na mwakilishi wa wanawake wa Kirinyaga Jane Njeri waliungana na wakulima kukashifu malipo duni.