WIKI YA LUGHA ZA KIAFRIKA: Mikakati ya kukuza matumizi ya Kiswahili Kenya ibuniwe

WIKI YA LUGHA ZA KIAFRIKA: Mikakati ya kukuza matumizi ya Kiswahili Kenya ibuniwe

NA BITUGI MATUNDURA

WIKI ya Lugha za Kiafrika katika mwaka wa 2022 inatoa fursa muhimu ya kutafakari masuala mengi kuhusu lugha zetu za kiasili, umuhimu na mustakabali wazo katika siku zijazo.

Huku likiwa na jumla ya mataifa 53, Afrika ndilo bara lenye nchi nyingi zaidi likilinganishwa na mabara mengine. Mataifa kadhaa ya Afrika yana mamia ya lugha mbalimbali, lakini zinazozungumzwa na watu wachache.

Hali hii inaibua taswira ya ‘watu wachache, lugha nyingi’. Kwa mfano, Cameroon ina takriban watu milioni 26, lakini ina zaidi ya lugha 250.

Je, wingi-lugha katika bara la Afrika ni balaa au neema? Kutokana na ukweli kwamba mataifa ya Afrika yalitawaliwa na koloni mbalimbali za Ulaya katika karne ya 20, athari za utawala huo bado zinaonekana na kufanana kutoka taifa moja hadi jingine.

Kwa mfano, mataifa yote barani Afrika yamezipa kipaumbele lugha za kigeni katika masuala yao ya kitaifa. Kuanzia kaskazini hadi kusini, mashariki hadi magharibi, lugha za bara Ulaya ndizo zinatumika kama lugha rasmi huku lugha za Kiafrika zikiwekwa pambezoni. Lugha hizi hutumiwa sana na watu – ingawa hazitambuliwi rasmi.

Aghalabu lugha za kigeni hutumiwa kufundishia katika mifumo mingi ya elimu.

Mojawapo ya sababu bayana zinazochangia lugha za kigeni kuendelea kutawala masuala mengi ya mataifa ‘huru’ barani Afrika ni kwamba, mchakato wa kupata uhuru kamili haukuwahi kukamilishwa.

Wasomi wa Kiswahili, kwa mfano, wametumia dhana ya ‘uhuru wa bendera’ kuelezea hali duni ya maisha na miundombinu licha kwamba nchi zetu zimekuwa huru kwa zaidi ya miongo mitano. Bendera imesalia kuwa ishara ya uhuru tu – na hakuna kingine cha mno.

Kenya, iliyo na takriban makabila 43 ina bahati kuwa na lugha ya Kiswahili. Kutokana na hali hii, kaulimbiu ya maadhimisho ya Wiki ya Lugha za Kiafrika – Lugha za Kiafrika: Nyenzo za Afrika Tunayoitaka- inafungamana vyema na juhudi za kimakusudi zinazofanyika Kenya kuhakikisha kwamba Kiswahili kinapata nafasi yake stahiki kama chombo cha kuunganisha Wakenya.

Mnamo 2010 kwa mfano, Kenya ilikikweza hadhi Kiswahili kwenye katiba yake, kuwa lugha rasmi sambamba na Kiingereza. Hatua hii bado inaendelea kufanyiwa kazi licha ya kuwepo changamoto nyingi.

Kiswahili kimetengewa nafasi maalum na kinatumiwa kwa marefu na mapana katika vyombo vya habari ndani na nje ya nchi. Gazeti la Taifa Leo linafanya kazi nzuri kwa kutumia mwelekeo wa kushirikisha taasisi za elimu ya viwango vyote nchini. Vituo vingi vya habari huandaa vipindi ambavyo vinahusu matumizi ya Kiswahili.

Ili kuhakikisha Kiswahili kinatumika katika nyanja zote kwa ufasaha, vyombo vya habari vinasisitiza mno hali ya uzalendo. Mkabala huu ni ngao muhimu mno ya kukabiliana na athari za kikoloni nilizozitaja awali katika makala haya.

Katika kutilia mkazo dhana ya ukombozi kutokana na kasumba za ukoloni, mwandishi na mkereketwa wa lugha za Kiafrika na tamaduni pendwa – Prof Ngugi wa Thiong’o anasema: “ Ikiwa unajua (kuzungumza na kuandika) lugha zote ulimwenguni na hujui lugha yako ya ‘mama’, huo ni utumwa; ikiwa unajua lugha yako ya ‘mama’ (lugha asilia) na kuongezea lugha zote nyingine za ulimwengu, huo ni uwezeshwaji (empowerment).

Kauli ya Prof Ngugi wa Thiong’o inaakisi hali halisi katika ulimwengu wa sasa –kwamba mumo kwa mumo katika kuzikumbatia lugha za kigeni, tutakuwa na uwezo zaidi ikiwa tutazipa umuhimu lugha zetu asilia.

Kwa hiyo, katika karne hii, mataifa ya Afrika yanapaswa kutafakari zaidi namna ya kuziona lugha zao kama bidhaa muhimu ambazo zinaweza kuuzwa kwa njia moja au nyingine kwa minajili ya kujipatia mapato.

Mitaala ya elimu nchini Kenya inapaswa kuangazia muumano uliopo baina ya Kiswahili na nafasi za ajira. Fursa zilizopo katika utumikishaji wa ya Kiswahili na lugha nyingine za kiasili ni nyingi – mradi tu sera ya lugha iimarishwe na kutekelezwa kikamilifu.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

  • Tags

You can share this post!

Apewa siku moja kurejesha pesa alizoibia mwajiri

Kalonzo sasa apanda bei

T L