Habari Mseto

Mikakati ya kutunzia wagonjwa wa corona nyumbani

June 11th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

Wizara ya Afya Jumatano ilizindua rasmi mikakati itakayotumika kuwatunza wagonjwa wa Covid – 19 nyumbani.

Serikali imechukua hatua hiyo ili kupunguza idadi ya juu ya wagonjwa wa virusi vya corona katika vituo vya afya nchini, inavyosema vimejaa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mikakati hiyo katika makao makuu ya Idara ya Afya, Waziri Msaidizi katika Wizara Dkt Rashid Aman alisema utunzaji wa wagonjwa wa Covid – 19 nyumbani ambao hawaonyeshi dalili za kuambukizwa na kutolemewa, unaruhusiwa na Shirika la Afya Duniani, WHO, mipangilio kabambe ikiwekwa.

Mikakati iliyozinduliwa ni pamoja na uhalali wa wasioonyesha dalili za ugonjwa huu na hawajalemewa, namna ya kuwatunza, matibabu watakayopewa, idhini ya kuwatunzia nyumbani, waliopona na uwepo wa jamii kuwakumbatia.

Akieleza mikakati ya kufanikisha mipango hii katika mitaa ya mabanda, Waziri pia alisema wahudumu wa afya wa kijamii wa kujiotolea watajumuishwa. Dkt Aman pia alisema mfumo wa Nyumba 10 utashirikishwa.

“Mikakati tuliyozindua ina maelezo kamilifu namna ya kutunza wagonjwa. Kwa mengi zaidi, imepakiwa katika tovuti ya wizara,” Waziri akasema.

Kulingana na Waziri, asilimia 78 ya takwimu za maambukizi ya Covid – 19 nchini, hawaonyeshi dalili wala dalili tata, hivyo basi wanaweza kutunziwa nyumbani kwa mujibu wa mikakati iliyozinduliwa ili kupunguza msongamano katika vituo vya afya na kuwezesha wahudumu wa afya kuhudumia waliolemewa.

“Hawaonyeshi dalili, wengine ni dalili chache kama vile homa isiyohitaji matunzo ya hospitali,” Dkt Aman akaeleza, akiongeza kusema kuwa mbali na kutunziwa nyumbani, pia kuna maeneo ya kijamii yatakayozinduliwa kuwahudumia.

Waziri alisema mikakati iliyozinduliwa itaanza kutekelezwa mara moja.

Barani Afrika, Kenya imejiunga na mataifa kama vile Nigeria na Afrika Kusini kutunza baadhi ya wagonjwa wa Covid – 19 nyumbani.

Mataifa hayo yamethibitisha idadi ya juu ya maambukizi ya virusi vya corona, ambavyo kwa sasa ni janga la ulimwengu mzima.

Aidha, mataifa ya ughaibuni yaliyoimarika kimaendeleo, yamekumbatia mkondo huo.

Kutokana na ongezeko la maambukizi ya Covid – 19, huenda mataifa mengi Barani Afrika yakafuata nyayo hizo ili kupunguza idadi ya juu ya wagonjwa katika vituo vya afya.