Lugha, Fasihi na Elimu

Mikakati ya kuzima wanafunzi wanaotumia ChatGPT kufanya udanganyifu

March 31st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KATIKA ulimwengu wa sasa ambapo mpenyo wa teknolojia unaendelea kushika kasi, wahadhiri katika vyuo vikuu tofauti nchini Kenya wameelezea wasiwasi wao kufuatia ongezeko la wanafunzi wanaotumia teknolojia ya ChatGPT kufanya udanyanyifu katika masomo yao.

Hii, wanasema, imelazimu vyuo kuanza kutafuta mikakati ya kuwazima wanafunzi wadanganyifu.

Wahadhiri wanasema kuwa wanafunzi wengi wanatumia teknolojia hiyo kufanya tafiti za kimasomo ikiwemo kuandaa tasnifu za shahada tofauti, kama vile uzamili na uzamifu.

“Wanafunzi wengi hawafanyi utafiti wa kutosha kuandaa tasnifu zao kama inavyotakikana. Badala yake, wengi wanatumia teknolojia ya ChatGPT kuandaa tasnifu hizo. Kile wanasahau ni kwamba matini mengi yanayoandikwa kwa teknolojia hiyo hayajafikia kiwango cha kiusomi kama inavyotakikana. Sababu ni kuwa, hayawezi yakarejelewa na pili, mengi huwa na makosa mengi hata ya kisarufi,” asema Dkt Joyce Kamuren, ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nazarene jijini Nairobi.

Kulingana na Dkt Kamuren, taaluma zilizoathiriwa sana na matumizi ya teknolojia hiyo ni zile za masomo ya kijamii, kwani huwa hazihusishi uwepo wa hisabati.

“Wanafunzi wengi hawasomi. Hata wakati wa mitihani, baadhi yao wamekuwa wakitumia teknolojia hiyo kupitia simu zao kufanya udanganyifu,” akasema Dkt Kamuren kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Hata hivyo, anaonya kuwa ni rahisi kuwanasa wanafunzi wanaotumia teknolojia hiyo kufanya udanganyifu, kwani wengi wao huwa hawapitii kikamilifiu matini wanayopata kupitia teknolojia hiyo.

Hivyo, anasema kuwa kwa wahadhiri wenye uzoefu, ni rahisi sana kuwanasa wanafunzi waliotumia njia hiyo kufanya udanganyifu, kwani baadhi ya vyuo vimeanza kuweka mikakati ya kubaini tasnifu zilizotayarishwa kupitia teknolojia hiyo, badala ya njia ya kawaida ya kiusomi.

“Katika chuo chetu, tumeweka mikakati ya kiteknolojia kuhakikisha tunawanasa wale wanaotumia teknolojia hiyo kuandaa tasnifu zao. Ushauri wangu kwa wanafunzi ni kuhakikisha wametia bidii masomoni, kwani watajisaidia sana katika siku za usoni,” akasema.

Mhadhiri mwingine, Dkt Rose Adhiambo, anasema kuwa vyuo kadhaa vimebuni vitengo maalum vya kukagua uhalali wa tasnifu zinazowasilishwa kwa wanafunzi wake—hasa katika kiwango cha shahada za uzamili na uzamifu.

“Kwa sasa, siwezi kuvitaja vyuo hivyo, ingawa kuna mikakati inayoendelea kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaotumia njia hizo kufanya udanganyifu wananaswa virahisi na kuchukuliwa hatua zifaazo za kinidhamu,” akasema.

Hilo linajiri wakati waajiri wengi nchini wameeleza wasiwasi wao kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofuzu kutoka vyuo vikuu bila ujuzi wa kutosha wa kozi walizosomea.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Waajiri Kenya (FKE), Bi Jacqueline Mugo, waajiri wengi wamekuwa wakilazimika kuwafunza upya wanafunzi ili kupata ujuzi unaofaa kabla ya kuwaajiri.

“Kwa kweli, baadhi ya waajiri wameeleza kwamba wamelazimika kuwafunza upya wanafunzi wanaofuzu kutoka vyuo vikuu na taasisi nyingine za masomo ya juu ili kupata ujuzi unaohitajika katika taaluma zao,” akasema.