Mikakati ya Nassir kufufua uchumi Mombasa

Mikakati ya Nassir kufufua uchumi Mombasa

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Mvita Bw Abdulswamad Nassir ambaye anagombea ugavana kaunti ya Mombasa kwa tiketi ya ODM, amewahakikishia wawekezaji wa utalii kuwa atafufua sekta hiyo kwa kupunguza ada za mahoteli na leseni.

Alisema uchumi wa Mombasa lazima ufufuliwe kupitia sekta ya utalii.

“Tutahakikisha washikadau wanafanya biashara bila ya kuhangaishwa, serikali yangu itashirikiana na mwekezaji ambaye ataweza kuwekeza katika sekta ya taka. Wahudumu wa ufuoni maarufu beach boys watapewa mafunzo katika vyuo vya kiufundi ili waweze kusajiliwa na kupewa ajira,” alisema Bw Nassir.

Akiongea katika mkutano wa washikadau kuhusu ufufuzi wa uchumi, Bw Nassir alisema atashirikiana na washika dau kuhakikisha usafi unadumishwa katika fuo za Mombasa ili kuzingatia mazingira bora.

Alisema Mombasa inafaa kuuzwa kama soko la kipekee huku akiwarai washika dau kuwekeza kwenye ukumbi maalum wa mikutano sawa na ule wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) jijini Nairobi.

“Hili linawezekana, wafanyibiashara wanapenda kuja Mombasa kufanya mikutano yao sababu ya mandhari bora, halafu baadaye wanaenda kuzuru maeneo ya kuvutia kama ufuoni. Mji wa Kale maarufu Old Town unafaa kuuzwa kama eneo la kitamaduni ambapo kuna hata vyakula vya Kiswahili,” alisema Bw Nassir.

Wawekezaji hao wamewataka viongozi wa maeneo ya Pwani na Nyanza kuishinikiza serikali kuu kufungua anga zake ili ndege za kimataifa zitue katika viwanja vya ndege vya kimaitaifa vya Moi Mombasa na Kisumu.

Waliwataka wanasiasa za maeneo hayo kuanza kujadili na uongozi wa serikali kuu ili viwanja hivyo vya kimataifa vya ndege zifufue sekta ya utalii ambayo ilidorora kufuatia janga la corona.Janga hilo lilipelekea sekta ya kimataifa ya utalii kudorora baada ya nchi za kimataifa kusitisha usafiri.

“Kama ndege hazitatua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi hapa Mombasa basi raslimali hiyo itakuwa haina maana. Serikali kuu imewekeza sana katika miundo misingi bora ya kuvutia watalii ikiwemo daraja la Makupa ambalo linanuiwa kuiweka Mombasa kuwa kisiwa,” alisema Bw Mohammed Hersi mtaalam wa Utalii.

Alisema daraja hilo ambalo linanuiwa kufunguliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kuondoka mamlakani Agosti 9, litapiga jeki utalii.

“Waziri wa Uchukuzi ameanza kuzungumzia swala la kufungua anga zetu, majuzi alitaja kampuni za ndege za KLM, Qatar na Turkish ambazo zinataka kuanza safari zake Mombasa. Hii ni dalili nzuri. Uongozi wa Pwani unatilia mkazo swala la bandari ilhali utalii ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu,” alisema.

Alisema Wajerumani na Wafaransa ni baadhi ya watalii wa kimataifa ambao wanapenda kuzuru Pwani ya Kenya lakini wanapitia changamoto kufuatia ukosefu wa ndege ya moja kwa moja.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa Homa Bay wataka Raila awapelekee minofu katika...

Jumwa amsifia Ruto, asema ndiye suluhu ya uchumi wa nchi...

T L