Mikakati ya serikali ilinusuru Kenya kwa corona – Uhuru

Mikakati ya serikali ilinusuru Kenya kwa corona – Uhuru

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta amesema kwamba mikakati ya serikali yake iliokoa nchi mwaka 2020, janga la corona lilipovuruga uchumi na kuathiri nchi nyingi ulimwenguni.

Alisema kwamba kupitia hatua za kukinga raia kutokana na athari za janga la corona ambazo serikali yake ilichukua, uchumi wa Kenya haukuporomoka kama wa baadhi za nchi ulimwenguni.

Kwenye hotuba yake ya hali ya taifa bungeni, Rais Kenyatta alisema kwamba mipango kama vile Kazi Mtaani na kupunguza viwango vya ushuru, kusaidia biashara kupitia kupunguza viwango vya riba ilisaidia kuokoa uchumi.

Alisema kwamba hatua za serikali yake zimefanya uchumi kuanza kufufuka huku Kenya ikiorodheshwa nchi ya sita tajiri barani Afrika.

Licha ya janga la corona kuathiri sekta kadhaa za uchumi, Rais alisema kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru KRA ilipitisha kiwango cha ushuru ilichokuwa imeweka kutoka Sh1.5 trilioni hadi Sh1.67 trilioni.

Alisema kwamba ni kufuatia ufanisi wa mipango hiyo alitangaza awamu ya tatu ya kufufua uchumi ikiwemo Kazi Mtaani, kufufua sekta za kilimo, mifugo na afya.

Katika awamu hiyo, Wakenya walioshindwa kulipa mikopo katika kipindi cha corona watapata afueni.

You can share this post!

Otieno achanja pasi muhimu AIK ikizoa ushindi muhimu Ligi...

Corona: Wakfu wa Aga Khan watoa msaada

T L