Habari Mseto

Mikasa bin balaa

April 24th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

NZIGE ndio walitangulia kutua Kenya Desemba 2019. Virusi vya corona vikafuata Machi, nayo mafuriko mabaya zaidi kwa miaka mingi yamefika Aprili. Ni mkasa baada ya mkasa!

Ziwa Victoria limejaa pomoni na maji yake kuanza kumwagika kwenye makao na mashamba ya kilimo.

Hapo jana ilibainika watu 23 hawajulikani waliko katika lokesheni ya Kipchumwa, Marakwet Mashariki ambako maporomoko yaliyoua zaidi ya watu 39 katika kituo cha biashara cha Chesegon yalianza wikendi. Wakazi walisema miili mitatu ilipatikana.

Kwa mara ya kwanza tangu uhuru, kafyu imewekwa Kenya yote kutokana na virusi vya corona huku watu wakipigwa marufuku kuingia na kutoka Nairobi, Mombasa, Kilifi, Kwale na Mandera.

Virusi hivyo kwa mara ya kwanza pia vimelazimisha kufungwa kwa makanisa na misikiti, mazishi ya watu wengi kuharamishwa, maeneo ya starehe kuzimwa na watu kulazimishwa kuvaa maski.

Pia kwa mara ya kwanza, Kenya imevamiwa na idadi kubwa zaidi ya nzige kuwahi kuonekana kwa zaidi ya miaka 70.

Kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), idadi ya nzige hao inazidi kuongezeka na kufikia hatua hatari kutokana na wadudu hao kuendelea kuzaana katika maeneo ya Kaskazini na Kati mwa nchi.

“Hii inatishia kuleta hali ambayo haijawahi kuonekana ya uhaba wa chakula,” yasema FAO kwenye ripoti yake ya Jumanne.

Wakazi wa Nyanza wanasema mafuriko yanayoshuhudiwa sasa hayajawahi kuonekana huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha Milima ya Nandi na Ziwa Victoria likivuja.

Kufikia sasa watu watano wamekufa Kaunti ya Kisumu kutokana na mafuriko hayo.

Mnamo Jumanne Mto Nyando ulivunja kingo na kusababisha mji wa Ahero kufurika hadi barabara kuu ya Kisumu-Nairobi.

Sasa wakazi wa vijiji vya Kakola Ombaka, Agoro na Kadhiambo katika kaunti ndogo ya Nyando wanasema hawajawahi kuona mafuriko mabaya kama ya sasa.

Kulingana na Naibu Chifu Lawrence Onyango wa Lela, zaidi ya familia 800 zimeathiriwa na mafuriko kijijini Kanyumba.

Magharibi mwa Ugenya katika Kaunti ya Siaya, zaidi ya watu 800 eneo la Sifuyo Magharibi wameathirika na mafuriko baada ya Mto Nzoia kuvunja kingo.

Mbunge wa Bondo Gideon Ochanda asema hali ni ya kusikitisha hasa kutokana na maji ya Ziwa Victoria kufurika mashambani hasa maeneo ya Yimbo.,

Tayari Daraja la Goye linalounganisha Ufuo wa Usenge na eneo la Osieko katika Bundalangi limefunikwa na maji.

Katika mradi wa mpunga wa Ahero, zaidi ya ekari 7,500 zilizokuwa na mimea ya mpunga zimefurika maji.

Wakulima hao walisema hawajawahi kuona mafuriko kiasi hicho tangu walipoanza kulima mpunga.

Tayari familia zaidi ya 8,500 zimeachwa bila makao.

Katika eneo la Elburgon, Kaunti ya Nakuru, wakazi wanakadiria hasara kubwa baada ya mafuriko kuharibu mimea, makanisa na nyumba baada ya Mto Ruro kuvunja kingo.

Barabara ya Elburgon – Ndoswa haipitiki na imetatiza usafiri kwa wakazi maeneo ya Ndoswa na Lawina

Katika Kaunti ya Nyandarua, Kamishna Boaz Cherutich ameagiza familia zaidi ya 400 katika kijiji cha Gachuha, eneobunge la Kipipiri kuhamia maeneo ya juu kutoka na hatari ya kijiji chao kufurika.

Tayari Mto Turasha umevunja kingo zake na kulazimu wakazi kupiga kambi katika Shule ya Msingi ya Gachuha.

Katika eneo la Nyandarua Kaskazini, mzee wa miaka 71 aliyetambuliwa kama John Gichuhi alisombwa na maji ya Mto Sabugo.

ijini Nairobi, Naibu Kamishna wa South ‘B’ Philip Mbuvi ameamuru zaidi ya familia 1,500 zihamie maeneo ya juu.

Wakazi hao ni wa mitaa ya mabanda ya Mariguini, Fuata Nyayo, Kenya Wine, Kisii, Maasai, Hazina na Mukuru- Kaiyaba.

Ripoti za Jared Nyataya, Victor Raballa, Dickens Wasonga, Rushdie Oudia, Elizabeth Ojina, John Njoroge, Steve Njuguna na Sammy Kimatu