Michezo

Mikataba ya wanaraga nchini yafutwa

April 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limesimamisha kandarasi zote za wachezaji wa timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, kutokana na virusi vya homa ya corona.

Kwa kawaida, mikataba ya wanaraga wote ambao huvalia jezi za Shujaa hutamatika Julai ya kila mwaka baada ya kukamilika kwa duru zote za kampeni ya Raga ya Dunia. Mchuano ujao kwa Shujaa katika ulingo wa raga ya kimataifa umeratibiwa kufanyika Septemba 2020.

Ilivyo, huenda KRU ikaamua pia kupunguza mishahara ya wachezaji wa Shujaa ambao wamepangiwa kuanza upya mazoezi mnamo Julai. Haya ni kwa mujibu wa mwenyekiti wa KRU, Oduor Gangla ambaye amefichua mipango ya kubadilisha michakato mbalimbali kuhusu namna raga ya humu nchini inavyoendeshwa.

Kutokana na hatua hiyo ya KRU, Paul Feeney ambaye ni kocha mkuu wa Shujaa, amerejea nchini kwao New Zealand kwa likizo ya miezi minne bila malipo. Hii ni kutokana na hali ngumu ya kifedha ambayo imekuwa ikikabili Shirikisho la Raga la Kenya kwa miaka kadhaa iliyopita.

Kwa mujibu wa ratiba ya Shujaa, kikosi hicho kinatarajiwa kurejelea mazoezi ya wiki nane mnamo Julai kabla ya kuanza kunogesha duru nne zilizosalia katika kampeni za Raga ya Dunia msimu huu mnamo Septemba.

Baada ya kushiriki duru za Paris, Ufaransa na London, Uingereza mnamo Septemba, Shujaa wataelekea Hong Kong, China kisha Singapore nchini Malaysia.

“KRU lazima itafute mbinu za kufanikisha uendeshaji wa timu ya taifa na kubuni mikakati ya muda mfupi na ya kudumu kuhusu jinsi raga ya humu nchini itakavyostawishwa. Itatulazimu kufanya maamuzi magumu na mazito ili kukabiliana vilivyo na hali ya sasa ya corona,” akasema Gangla katika kauli iliyosisitizwa na Katibu Mkuu wa KRU, Ian Mugambi.

Bajeti ya kikosi cha Shujaa mwaka huu ilikadiriwa kufikia kati ya Sh60-70 milioni, fedha hizi zikijumuisha mishahara, marupurupu, ada za kambi za mazoezi, chakula na gharama nyinginezo.

Kuhusiana na utaratibu wa jinsi ujira wa wanaraga wa Shujaa hutolewa, nahodha Andrew Amonde, nyota Collins Injera, Oscar Ouma, Willy Ambaka na Billy Odhiambo ndio hupokezwa mishahara ya juu zaidi kutokana na urefu wa muda ambao wamehudumia timu ya taifa.

Kundi la pili la wanaraga ambao wamewajibikia Shujaa kwa kati ya miaka saba na nane ni lile linalowajumuishwa Dan Sikuta, Nelson Oyoo, Bush Mwale, Alvin ‘Buffa’ Otieno, Sammy Oliech na Jeff Oluoch ambaye ni nahodha msaidizi.

Kundi la tatu la wachezaji wanaopokea mishahara midogo ikilinganishwa na wenzao kwa sababu ya uchache wa miaka ambayo wamevalia jezi za Shujaa ni Johnstone Olindi, Vincent Onyala, Daniel Taabu, Herman Humwa, Geoffrey Okwach na wengineo.

Kufikia sasa, Shujaa wanashikilia nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la Raga ya Dunia kwa alama 35 na wamefikia robo-fainali za Main Cup mara mbili msimu huu.