Makala

'Mikebe ya plastiki badala ya kutupwa ovyo yaweza kutumika tena'

August 28th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

KADRI miaka inavyozidi kusonga ndivyo idadi ya watu inaendelea kuongezeka nchini.

Miaka 30 iliyopita ikilinganishwa na sasa kuna tofauti kubwa sana kiidadi ya wananchi. Hii inatokana na ongezeko la watu ambalo linaendelea kushuhudiwa kila uchao.

Familia zinapanuka, waliozaliwa miongo hiyo mitatu iliyopita nao wakijiunga na jahazi la uzazi.

Ongezeko la idadi ya watu ni suala lisilochangia mahitaji yaongezeke kuanzia lishe, makazi, mavazi, matibabu na elimu, haya yakiwa yale muhimu zaidi kuzingatia.

Mzazi au wazazi wana jukumu kuhakikisha meza haikosi kapu la mlo na kinywaji.

Hitaji hili linategemea sekta ya kilimo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa Kenya.

Chakula kinatoka shambani, na mifugo sharti ilelewe ardhini.

Ni wazi idadi ya watu inapoongezeka mashamba yanasalia yalivyokuwa tangu jadi.

Wataalamu wanasema kuna haja wananchi kukumbatia mifumo mipya kuzalisha chakula, uhaba wa ardhi chini ya kilimo na ufugaji ukiendelea kushuhudiwa.

Jessica Mbaka kutoka taasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo) anasema kuimarika kwa teknolojia kumejiri na njia mbadala za kuzalisha mazao pasi kutumia kipande kikubwa cha ardhi chini ya kilimo.

“Kivungulio (greenhouse) ni mojawapo wa mfumo tunayopendekeza wakulima wavalie njuga. Kinahitaji sehemu ndogo ya shamba,” asema afisa Jessica.

Isitoshe, kilimo cha mahema kinapunguza athari za wadudu na magonjwa, kwani kivungulio kimeezekwa.

Jessica anaendelea kueleza kwamba mkulima anaweza kijiundia kivungulio chake kwa kutumia vifaa vya gharama nafuu.

“Kinachohitaji ni miti au vyuma vya kukisimamisha, karatasi ngumu ya nailoni na chandarua na misumari,” asema.

Hata hivyo, ulijua baadhi ya vifaa vya plastiki vinatumika katika kuzalisha mazao?

Vifaa vya kupakia au kuhifadhia mafuta pamoja na mitungi ya maji, ni baadhi ya vinavyoweza kutumika kukuza mimea.

Hope Wanjiru, mkulima Kiambu anasema vifaa hivyo kwake ni dhahabu.

“Huvikusanya na kuvitumia katika kilimo cha mboga kama vile spinachi na sukuma wiki. Pia huvikuzia matunda,” adokeza mwanadada Wanjiru.

Baada ya kuvitumia, baadhi ya watu hiviteketeza kwa ndimi za moto, ambapo ni hatari katika uchafuzi wa mazingira.

Kulingana na mkulima Wanjiru halmashauri ya kitaifa ya mazingira, Nema, inaruhusu ukuzaji wa mimea kupitia vifaa hivyo hasa vihifadhio vya bidhaa za kula.

“Idadi ya watu inaongezeka, hivyo basi mashamba ni haba. Mfumo wa vifaa vya plastiki umekumbatiwa na mataifa ya ughaibuni yaliyoimarika kiteknolojia na kiuchumi. Ni rahisi kuhidhibiti wadudu na magonjwa kupitia vifaa hivyo kwa njia za kiasili, jambo ambalo linachangia kudumisha kilimohai,” afafanua.

Ni mfumo ambao umeonekana kushika kasi maeneo ya mjini, baadhi ya watu wakifanya kilimo katika nyumba za kupangisha.

Aidha, vinawekwa katika veranda au nafasi iliyo ‘pweke’, kibarua kikiwa kunyunyizia maji.

Ni wajibu wa Nema ikiendelea kufanya msako wa viwanda vinavyochafua mazingira, ifanye hamasisho la utumizi wa vifaa vya aina hiyo.

Ikimbukwe, vinapotupwa na kutapakaa katika mazingira havichangii kuleta uchafu pekee bali pia ni mafichio au makazi ya wadudu hatari kama vile mbu. Mbu ni mdudu anayechangia katika usambaaji wa ugonjwa wa Malaria.

Hamasisho likifanywa kwa ushirikiano na wadau husika katika sekta ya kilimo, mbali na kukabili hatari ya maambukizi ya magonjwa, mazingira yatahifadhiwa pamoja na kuongeza kiwango cha mazao ya kilimo chini.