Jamvi La Siasa

MIKIMBIO YA SIASA: Sukari ya Magharibi kiazi moto kwa Ruto

February 4th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

MPANGO wa serikali wa kufufua sekta ya sukari Magharibi mwa Kenya ambao Rais William Ruto alitaraji kuutumia kujijenga kisiasa sasa unaonekana kuchochea ukaidi dhidi yake.

Hii ni baada ya wanasiasa wa eneo hilo, wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, kupinga ubinafsishaji wa viwanda vya sukari vya serikali; haswa kile cha Nzoia.

Viwanda vingine ambavyo serikali inapanga kukodisha kwa wawekezaji wa kibinafsi ni Chemelil, Miuhoroni, Miwani na kile cha SoNy kilichoko Awendo katika Kaunti ya Migori.

Mnamo Alhamisi, Rais Ruto, ambaye anafanya ziara ya kikazi ya siku tano katika kaunti za Bungoma, alipigwa na butwaa pale Bw Wetang’ula na wabunge wa Bungoma walisisitiza kuwa sharti wahusishwe “kikamilifu” katika mpango wa ubinafsishaji wa kiwanda cha Nzoia kwani “ndicho johari ya watu wetu.”

“Viongozi kutoka kaunti hii kuanzia Madiwani, Wabunge, Seneta, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake na Gavana na uongozi wa muungano wa wakulima wa miwa wa Nzoia sharti wahusishwe katika mpango mzima wa ubinafsishaji,” akasema spika Wetang’ula ambaye amehudumu kama seneta wa Bungoma kwa miaka 10, kati ya 2013 na 2022.

Kwa upande wake, mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga amemtaka Rais Ruto kukifufua kiwanda hicho na kuhakikisha Sh54 bilioni ambazo kampuni hiyo inadaiwa na wakulima, wafanyakazi na wadeni wengine, zimelipwa alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tulipohudhuria kongamano la kiuchumi katika eneo la Matisi, Bungoma kabla ya uchaguzi ya Agosti 9, 2022, rais aliahidi kununua mashine mpya ya kusaga miwa katika kiwanda cha Nzoia kwa muda wa siku 100 baada ya kuingia Ikulu. Lakini sasa anataka tuunge mkono mpango wa kukiuza siku chache baada ya wawekezaji kufanya ziara ya kukikagua ili wakikodeshe kwa miaka 30. Haya ni makosa,” akaeleza.

Lakini huku Rais akionekana kukwepa dhoruba kutoka kwa Bw Wetang’ula na wabunge wa mrengo wake wa Kenya Kwanza, alionekana kuelekeza hasira zake kwa wabunge wa upinzani kutoka eneo hilo.

“Nyinyi wabunge wa upinzani mnaopinga mpango wa serikali wa kufufua kiwanda hiki na sekta ya miwa mkae kando kwa sababu hamuelewi manifesto yetu. Hamkunipigia kura na hivyo, msivuruge mipango yetu,” akafoka huku akimjibu Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, wa chama cha Democratic Action Party-Kenya (DAP-K).

Lakini ni kinaya kwamba Spika Wetang’ula na wabunge wa Kenya Kwanza kutoka eneo hilo wanapinga ubinafsishaji wa viwanda vya sukari ilhali ni wao waliwezesha kupitishwa kwa marekebisho ya Sheria ya Uwekezaji ya 2023, sheria inayompa Waziri wa Fedha usemi mkubwa katika ubinafsishaji wa mashirika ya serikali.

Wadadisi wa kisiasa sasa wanaonya kuwa suala hilo ni kiazi moto ambacho Rais Ruto anapasa kushughulikia kwa uangalifu mkubwa mnamo.

“Spika Wetang’ula amediriki kumkaidi Rais kuhusu suala hilo baada ya kung’amua kuwa kinaweza kuzika ndoto zake za kisiasa. Hii ni kwa sababu kilimo cha miwa ni mojawapo ya nguzo za uchumi wa kaunti ya Bungoma na eneo la Magharibi kwa ujumla,” akasema Bw Martin Andati.

“Na ikumbukwe kuwa Bw Wetang’ula hajaficha azma yake ya kutaka kuwania urais 2032 endapo Rais Ruto atafaulu kukamilisha mihula yake miwili uongozini. Hii ndiyo maana anachukulia suala hilo kwa uzito,” anaongeza.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Rais Ruto alizoa jumla ya kura 229, 409 kutoka kaunti ya Bungoma akifuatwa kwa umbali na Raila Odinga wa Azimio aliyepata kura 13, 478 pekee.

Ikizingatiwa kwamba Dkt Ruto alimshinda Odinga kwa kura 209, 234 pekee kote nchini, Bw Wetang’ula amekuwa akikariri kila mara kwamba kura alizopata katika kaunti ya Bungoma ndizo zilimpa ufunguo wa Ikulu.