Kimataifa

Mikosi yaandama Haiti Waziri Mkuu mpya akipatwa na matatizo ya kupumua

June 11th, 2024 1 min read

PORT-AU-PRINCE, HAITI

NA MASHIRIKA

WAZIRI mkuu mpya wa Haiti, Garry Conille, aliondoka hospitalini Jumapili akiwa katika hali nzuri baada ya kulazwa akiwa na tatizo la kupumua siku mbili zilizopita.

Conille kupitia kanda ya video, Jumapili alasiri alionekana, akihutubia kupitia kwa video akiwa amesimama, akiwaambia watazamaji: “Ninachapisha video hii ili kuwahakikishia kuwa sijambo.”

Kulingana na mdokezi kutoka kwa serikali, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, hapo awali aliambia wanahabari kwamba waziri mkuu aliathiriwa na pumu.

Conille, 58, aliteuliwa kuwa waziri mkuu na Baraza la Mpito Haiti mnamo Mei 29 na kuapishwa Jumatatu iliyopita.

Kazi iliyo mbele yake ni kubwa sana ikiwemo kujizatiti kumaliza mizozo ya kisiasa, kuyakabili masuala ya kiusalama na kibinadamu.

Masuala hayo tata ndiyo wachanganuzi wa siasa wanasema yanaangamiza nchi hiyo maskini zaidi katika eneo la Magharibi bila kusahau jukumu la kuweka mikakati katika harakati za kufanya uchaguzi wa kwanza tangu 2016.

“Baada ya wiki ya shughuli nyingi, Conille aliugua ugonjwa kidogo mchana wa Jumamosi Juni 8, 2024, na akapelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu,” taarifa ya ofisi ya mawasiliano ya Waziri Mkuu ilisema Jumamosi.

Conille, ambaye kadhalika ni daktari wa matibabu kitaaluma, alihudumu kama waziri mkuu wa Haiti kwa kipindi kifupi mwaka 2011-2012, na hadi hivi majuzi alikuwa mkurugenzi wa kikanda wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF.

Tangu ateuliwe kuwa waziri mkuu, amekuwa akifanya msururu wa vikao na wadau na wawakilishi, huku akishirikiana na baraza hilo katika kuunda baraza la mawaziri.

Katika video yake Jumapili, Conille aliahidi kuwa baraza lake la mawaziri litakamilika wiki hii.

Ghasia za magenge kwa muda mrefu zimeikumba Haiti, lakini mwishoni mwa Februari, makundi yaliyojihami kwa silaha yalianzisha mashambulizo yaliyoratibiwa kwenye maeneo yaliyolengwa eneo la Port-au-Prince, yakidai yalitaka kumpindua waziri mkuu ambaye hakuchaguliwa na asiyependwa na watu wengi, Ariel Henry.