Habari Mseto

Mikutano yote nchini yazimwa ikiwemo ya BBI

March 13th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imepiga marufuku mikutano yote ya hadhara kote nchini kwa kipindi cha siku 30 kufuatia kugunduliwa kwa kisa cha kwanza cha COVID-19 nchini.

Hii inamaanisha kuwa mkutano wa uhamasisho wa Mpango wa Maridhiano (BBI) uliopangwa kufanyika Nakuru mwishoni mwa wiki ijayo na mikutano ya krusedi iliyopangwa maeneo tofauti nchini imesitishwa mara moja.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe pia alisema michezo baina ya shule na makongamano yote yamezimwa mara moja. Vilabu vya burudani haswa katika miji mikubwa ambavyo huvutia watu wengi pia vimeathiriwa na amri hii.

Hata hivyo, makanisa, misikiti, na taasisi za masomo zitaendelea na shughuli zao lakini zimeagizwa kuweka mitambo ya kuwawezesha watu kusafisha mikono.

“Tumesimamisha kwa muda mikutano yote ya hadhara, makongamano, krusedi, michezo na shughuli zozote ambazo zinaweza kuwaleta watu wengi pamoja wakati mmoja. Lakini ibada za kawaida za makanisa zinaweza kuendelea ila wanaoingia katika majumba ya ibada wawekewe vifaa vya kuosha mikono,” Bw Kagwe akaamuru.

Hii ina maana kwamba mkutano wa kutoa uhamasisho kuhusu ripoti ya Mpango wa maridhiano (BBI) uliotarajiwa kufanyika mjini Nakuru mnamo Jumamosi wiki ijayo sasa hautafanyika.

Kulingana na Waziri Kagwe, amri yake ya imeathiri mikutano yote ya hadhara nchini “bila kujali hadhi ya waandalizi na wahusika katika mikutano au makongamano husika.”

Ina maana kwamba amri hiyo pia imeathiri mikutano ya kuchanga fedha kwa kufadhili miradi mbalimbali ambayo Naibu Rais William Ruto amekuwa akihudhuria maeneo mbalimbali kuvumisha azma yake ya kuwania urais 2022 pia imezimwa kwa siku 30.

Mkutano wa BBI ulikuwa umepangwa kufanyika katika uwanja wa michezo wa Afraha mnamo Machi 21 baada ya mkutano mwingine kama huo kufanyika Meru Jumamosi iliyopita.

Mnamo Jumatano wiki hii Rais Uhuru Kenyatta alifanya kikao na magavana tisa kutoka eneo la Rift Valley kujadili mipango ya mkutano huo.

Mnamo Alhamisi, kundi la wabunge na maseneta kutoka eneo hilo walitangaza kuwa wao ndio watausimamia mkutano huo wala sio watu sio viongozi waliowataja kama “wageni.”

“Nakuru ni kitovu cha amani kwani hapo ndipo chama cha Jubilee kilibuniwa. Wageni wamealikwa lakini hatutawaruhusu kuendeleza siasa za matusi katika mkutano huo kwani hiyo itakuwa siku ya kuangazia masuala yanayowahusu wakazi wa Rift Valley,” akasema seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.

Kando na mikutano ya hadhara, Waziri Kagwe pia alitangaza kuwa watu wa kawaida hawataruhusiwa kutembelea magereza yote nchini kwa kipindi cha siku 30 zijazo.

“Hii ni baadhi ya mikakati ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo,” akasema kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Kutokana na marufuku hii, kumbi na vilabu vingi ambako mikutano na makongamano huandaliwa hasa katika miji mikubwa nchini zitapata hasara kwa kukosa wateja.

Wanasiasa nao watakosa majukwaa ya kuchapa siasa kama ambavyo imekuwa kawaida yao siku ya wikendi kila wiki. Ratiba ya michezo shuleni katika muhula huu wa kwanza pia imevurugwa.