Habari

Milango ya mjadala kuhusu BBI imefungwa, Ruto aambiwa

November 2nd, 2020 1 min read

Na WAANDISHI WETU

JUHUDI za Naibu Rais, William Ruto za kutaka mdahalo wa kitaifa kuhusu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), zimegonga mwamba baada ya wandani wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kumpuuza na kusema milango ya kuijadili imefungwa.

Rais Kenyatta na Bw Odinga pia wamenyamazia wito huo na inasemekana wameanza mikakati ya kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kura ya maamuzi.

Wakizungumza maeneo tofauti mwishoni mwa wiki, wabunge wanaounga ripoti hiyo walisema wako tayari kwa kura ya maamuzi ili waipitishe.

Wakiongozwa na Mbunge Maalum Maina Kamanda wabunge wapatao 20, walitaja pendekezo la kuifanyia ripoti hiyo marekebisho zaidi kama la kuwapotezea wakati Wakenya wenye kiu ya kuipitisha

“Naibu Rais na watu wake walikataa kuwasilisha maoni na mapendekezo yao kwa jopo kazi la BBI lakini sasa wanatusumbua eti wanataka ripoti hiyo ibadilishwe ili kuingiza matakwa yake. Hatutaruhusu hilo,” akasema Bw Kamanda.

Akaongeza: “Ningependa kumwambia William Ruto na wenzake, nafasi walipewa na wakaipoteza. Sasa kuanzia Jumatatu (leo) tunaanza kukusanya sahihi ya kufanikisha kura ya maamuzi kuhusu BBI na tuna uhakika kwamba hapa Nairobi pekee, tunaweza kupata zaidi ya sahihi milioni moja.”

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino pia ndiye alipinga wazo la kufanyia marekebisho ripoti hiyo akilifananisha na njama ya kuwakosesha Wakenya manufaa yaliyomo.

Wabunge hao walikuwa wakiongea Jumapili katika Kanisa la Friends Church Quaker Kabete, Nairobi ambako walihudhuria ibada ya Jumapili.

Naye mbunge wa Tiaty, William Kamket alimkashifu vikali Naibu Rais Dkt William Ruto kwa kupendekeza mabadiliko yafanyiwe ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) iliyozinduliwa wiki moja iliyopita.

Bw Kamket ambaye ni mwandani wa Seneta wa Baringo Gideon Moi, alisema Dkt Ruto alifaa kuwasilisha mapendekezio yake wakati wanachama wa jopo hilo walikuwa wakikusanya maoni kutoka kwa raia kote nchini.

CHARLES WASONGA, BENSON MATHEKA na FLORA KOECH