Kimataifa

Milioni 1.5 wameambukizwa corona Afrika – kituo chaeleza

October 6th, 2020 2 min read

Na XINHUA

ADDIS ABABA, Ethiopia

IDADI ya visa vya watu waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona barani Afrika imefikia milioni 1.5, takwimu za Taasisi ya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi (CDC) Afrika, zimeonyesha.

CDC Afrika jana ilisema kuwa visa vya corona vimefikia 1,506,185 huku idadi ya waliofariki kutokana na maradhi hayo hatari ikiwa 36,614.

Taasisi hiyo ilisema kuwa watu 1,243,259 waliokuwa na virusi vya corona wamepona.

Mataifa ya Afrika yaliyoathiriwa zaidi na idadi ya juu ya watu walioambukizwa virusi vya corona ni Afrika Kusini, Morocco, Misri, Ethiopia na Nigeria mtawalia.

Mataifa ya Kusini mwa Afrika ndiyo yameathirika zaidi kwa kuwa na idadi kubwa ya visa na vifo vilivyotokana na maradhi ya corona.

Mataifa ya Kaskazini Mashariki mwa Afrika ni ya pili kwa kuwa na visa vingi na maafa yaliyosababishwa na corona. Ni mataifa matatu tu ya Afrika ambayo yameripoti visa zaidi ya 100,000.

Nchi ya Afrika Kusini ambayo imethibitisha jumla ya visa 679,716 ndiyo imeathiriwa zaidi barani Afrika. Watu 16,938 wamefariki kutokana na virusi vya corona nchini humo.

Morocco ambayo imethibitisha visa 131,228 na kupoteza watu 2,293 inafuatia.

Misri imethibitisha visa 103,575 vya waathiriwa wa virusi vya corona na kati yao 5,970 wameaga dunia.

Jumla ya visa vya maambukizi barani Afrika ni sawa na asilimia 4.4 ya visa vya waathiriwa wa virusi vya corona ambavyo vimethibitishwa kote duniani.

Taasisi ya Africa CDC ilisema kuwa mataifa 12 barani Afrika yamekuwa yakiripoti idadi ya juu ya vifo kuliko wastani wa kimataifa wa asilimia tatu.

Mataifa hayo yanayoripoti idadi ya juu ya vifo vya corona kuliko wastani wa kimataifa ni pamoja na Chad, Liberia, Niger, Misri, Mali, Angola, Algeria na Sudan.

Bara la Afrika limechangia asilimia 3.6 ya vifo vinavyosababishwa na virusi vya corona kote duniani kwa mujibu wa CDC Afrika.

Awali, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikuwa limetabiri kuwa bara la Afrika lingeshuhudia maafa ya mamilioni ya watu kutokana na janga la virusi vya corona.

Lakini kufikia sasa, bara la Afrika ndilo limepata nafuu ikilinganishwa na mabara mengine kama vile Ulaya, Amerika na Asia.

Watafiti wamekuwa wakikuna vichwa katika juhudi za kutegua kitendawili kuhusu idadi ndogo ya visa vya corona barani Afrika.

Baadhi ya wataalamu sasa wanasema kuwa Afrika imekuwa na ujuzi mkubwa katika kukabiliana na maradhi hatari kama vile Ebola, malaria na kadhalika.

Watafiti wengine wanasema kuwa idadi kubwa ya watu barani Afrika ni wa umri mdogo tofauti na mataifa ya Ulaya yaliyo na idadi ya juu ya wazee.

Asilimia 40 ya watu barani Afrika ni watoto walio chini ya umri wa miaka 14.