Michezo

Aguero kuanza tena kuwajibishwa na Man-City baada ya mechi za kimataifa

November 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amethibitisha kwamba fowadi matata Sergio Aguero atarejea kikosini baada ya likizo fupi ya Novemba itakayoshuhudia kipute cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kikipisha michuano ya kimataifa kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Aguero, 32, alipata jeraha la paja mnamo Oktoba, 2020 akichezea waajiri wake katika EPL dhidi ya West Ham United. Jeraha hilo limemweka nje ya mechi mbili zilizopita za Man-City.

Hata hivyo, Guardiola ameshikilia kwamba hatakuwa mwepesi wa kumwajibisha nyota huyo mzawa wa Argentina uwanjani. Aguero alipata jeraha analoliuguza kwa sasa baada ya kupiga mechi moja pekee tangu ajipate mkekani kwa kipindi kirefu baada ya kuumia goti.

“Nina hakika kwamba atakuwa sawa kabisa baada ya likizo fupi ijayo. Anaendelea vyema japo haitakuwa busara kumchezesha mapema jinsi tulivyofanya Oktoba,” akasema mkufunzi huyo raia wa Uhispania ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Bayern Munich na Barcelona.

Gabriel Jesus ambaye ni fowadi mwenza wa Aguero kambini mwa Man-City alirejelea mazoezi mnamo Novemba 1, 2020 kwa minajili ya gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) litakalowakutanisha na Olympiakos mnamo Novemba 3.

Kufikia sasa, Man-City wanaongoza Kundi C baada ya kushinda FC Porto na Olympique Marseille za Ureno na Ufaransa mtawalia katika mechi mbili za ufunguzi.

“Kinyume na hali ilivyo miaka 10 iliyopita, ni vigumu sana kwa sasa kusonga mbele kwenye gozi la UEFA kuanzia hatua ya makundi. Kila kikosi kwa sasa kina kiasi kikubwa cha fedha na klabu zinajinasia huduma za wanasoka wa haiba kubwa kutoka kote duniani,” akasema Guardiola.

Kati ya chipukizi ambao Gaurdiola amekweza ngazi kucheza katika kikosi chake cha kwanza baada ya kuumia kwa Aguero, Benjamin Mendy na Jesus ni pamoja na Liam Delap, Taylor Harewood-Bellis, Cole Palmer na Tommy Doyle.

Chipukizi hao walitarajiwa kuwa sehemu ya kikosi ambacho Guardiola angetegemea dhidi ya Chelsea kwenye fainali ya Youth Cup mnamo Novemba 2, 2020 uwanjani St George’s Park, Uingereza. Man-City walitwaa ubingwa wa kivumbi hicho kwa mara ya kwanza mnamo 2008 na walitegemea sana huduma za masogora Ben Mee, Kieran Trippier na Daniel Sturridge wakati huo.