Michezo

Milner mchezaji wa 11 kushinda EPL akiwa klabu tofauti

July 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

UFANISI wa Liverpool wa kunyanyua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kusubiri kwa miaka 30 uliwawezesha kuandikisha historia katika viwango mbalimbali.

James Milner ni miongoni mwa wanasoka waliondikisha historia pindi baada ya nahodha wa Liverpool Jordan Henderson kunyanyua ufalme wa kombe la EPL mnamo Julai 22, 2020 kufuatia ushindi wao wa 5-3 dhidi ya Chelsea uwanjani Anfield.

Milner, 34, alijiunga na orodha ya wachezaji 11 wengine ambao wamejizolea ubingwa wa taji la EPL wakivalia jezi za vikosi tofauti.

Milner alikuwa sehemu ya kikosi cha Manchester City kilichotwaa ubingwa wa EPL mnamo 2011-12 na 2013-14. Baada ya kuongoza miamba hao kufikia mafanikio hayo, Milner ambaye ni kiungo tegemeo wa timu ya taifa ya Uingereza, aliondoka uwanjani Etihad mwishoni mwa msimu wa 2014 bila ada yoyote na kutua uwanjani Anfield kuvalia jezi za Liverpool mnamo 2015.

Licha ya kocha Jurgen Klopp kumwajibisha katika mechi chache tu na kumpanga sana katika kikosi cha wanasoka wa akiba muhula huu, mchango wa Milner umehisika pakubwa ndani na nje ya uwanja.

WANASOKA AMBAO WAMENYANYUA TAJI LA EPL WAKICHEZEA KLABU MBILI TOFAUTI

o James Milner – Manchester City na Liverpool

o N’Golo Kante – Leicester City na Chelsea

o Riyad Mahrez – Leicester City na Manchester City

o Robert Huth – Chelsea na Leicester City

o Nicolas Anelka – Arsenal na Chelsea

o Carlos Tevez – Manchester United na Manchester City

o Gael Clichy – Arsenal na Manchester City

o Kolo Toure – Arsenal na Manchester City

o Ashley Cole – Arsenal na Chelsea

o Mark Schwarzer – Chelsea na Leicester City

o Henning Berg – Blackburn Rovers na Manchester United