Michezo

Milner mtemi wa soka ambaye ana hela mithili ya changarawe

May 20th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

JAMES Milner, 33, ni winga matata mzawa wa Uingereza ambaye ushawishi wake unazidi kuhisiwa pakubwa kambini mwa Liverpool chini ya kocha Jurgen Klopp.

Ubunifu na maarifa yake uwanjani yamewahi kumwezesha kuziwajibikia klabu mbalimbali zinazopiga soka ya Uingereza zikiwemo Leeds United, Newcastle United, Aston Villa na Manchester City.

Uwezo wake wa kudhibiti mpira kwa miguu yote miwili, kuwapiga wapinzani chenga za maudhi na kutamba katika idara yoyote ugani ni sababu ambayo huwaweka makocha wake katika ngazi za klabu na timu ya taifa kumwajibisha mara kwa mara kama kiungo mvamizi.

UTAJIRI

Kufikia sasa, thamani ya mali ya Milner inakadiriwa kufikia kima cha Sh4.2 bilioni. Haya ni kwa mujibu wa Jarida la The Celebrity. Kiini kikubwa cha utajiri wake ni mshahara wa zaidi ya Sh950 milioni ambao kwa sasa anatia mfukoni mwishoni mwa kila mwaka uwanjani Anfield.

Kiasi hicho cha fedha ni maradufu ya ujira aliokuwa akidumishwa nao wakati akiwatandazia soka Aston Villa zaidi ya miaka 10 iliyopita kabla ya Man-City kuzihemea huduma zake mnamo Agosti 2010.

Kiasi cha pesa ambazo Milner anajirinia kwa sasa kambini mwa Liverpool kinamweka katika kikoa kimoja na Mohamed Salah na Virgil Van Dijk ambaye kwa sasa ndiye beki ghali zaidi katika ulimwengu wa soka.

Migongo ya masogora hawa watatu ambao ndio wanaodumishwa kwa mishahara ya juu zaidi kambini mwa Liverpool, inafuatwa kwa karibu na Dejan Lovren, Georginio Wijnaldum, Alex Oxlade-Chamberlain, Sadio Mane, Roberto Firmino na nahodha Jordan Henderson.

Mbali na kuwa balozi wa miradi mbalimbali inayopania kutambua na kukuza vipaji vya chipukizi katika soka nchini Uingereza, Milner pia hujirinia fedha za ziada kutokana na marupurupu na bonasi za kushinda mechi akivalia jezi za timu ya taifa na na klabu ya Liverpool inayoshuhudia ufufuo mkubwa katika soka ya ? Uingereza chini ya Klopp.

Kwa pamoja na Mario Goetze, Luka Modric, Sergio Ramos, Diego Godin na Robert Lewandowski, Milner pia ni balozi wa kutangaza bidhaa za kampuni ya Electronic Arts (EA Sports) ambayo humkabidhi takriban Sh35milioni kila mwezi.

Mnamo 2018, alitia saini kandarasi mpya ya miaka miwili na Liverpool katika maelewano yatakayompa ulazima wa kuendelea kutoa huduma zake ugani Anfield chini ya Klopp hadi mwishoni mwa 2020 huku akitazamiwa kuyoyomea Marekani au China mwishoni mwa kampeni za EPL muhula ujao.

MAGARI

Milner anamiliki magari mengi ya kifahari ambayo ni pamoja na BMW X6 M, Ferrari F12 Berlinetta, Mercedes CL63 AMG, Ferrari458, Audi RS7 na Range Rover Vogue. Thamani ya michuma hiyo inayosukumwa na winga huyo mkongwe inakisiwa kufikia kima cha Sh145 milioni. Mke wake, Amy Fletcher, aghalabu huendesha gari aina ya Ferrari 458 ambalo lilimgharimu Milner kima cha Sh22 milioni mnamo 2015.

MAJENGO

Milner anamiliki maskani ya kuvutia sana jijini London, Uingereza anakoishi na familia yake kila mara anapokuwa kazini. Pia ana jengo la kifahari zaidi mjini Wortley, Leeds, Uingereza wanakoishi wazazi wake. Mwishoni mwa 2016, Milner aliwajengea wazazi wake kas- ri la pili lililomgharimu Sh320 viungani mwa mji wa Chesire, Uingereza.