Mimba za mapema zapungua

Mimba za mapema zapungua

Na MAUREEN ONGALA

WASICHANA wengi walio chini ya umri wa miaka 20 katika Kaunti ya Kilifi wameanza kutumia mbinu za kupanga uzazi.

Aidha, idadi ya wanawake wanaotumia mbinu za kupanga uzazi imeongezeka kutoka asilimia 32 hadi asilimia 50.Afisa anayesimamia Afya ya Uzazi katika Kaunti ya Kilifi, Kennedy Miriti alisema hatua ya wasichana kukubali upangaji uzazi imepunguza idadi ya mimba za mapema.

“Wasichana wachanga wameanza kutumia aina mbalimbali ya upangaji uzazi. Miongoni mwa wanawake wote wanaotumia mbinu za kupanga uzazi, asilimia 38 ni vijana chipukizi wenye umri wa chini ya miaka 20,” alisema.Bw Miriti alisema mnamo 2014, Kilifi ilikuwa miongoni mwa kaunti 16 zilizoandikisha idadi ya chini zaidi ya wanaotumia mbinu za kupanga uzazi.

Kulingana na utafiti uliofanywa, ni asilimia 32 tu ya wanawake walio katika umri wa kupata watoto waliokuwa wakitumia mbinu za kupanga uzazi.“Idadi hiyo imeongezeka. Kuna tafiti kadhaa ambazo zimefanywa zinazoonyesha kuwa tumefikia asilimia 50 ya matumizi ya upangaji uzazi miongoni mwa wanawake walio katika umri wa kupata watoto,” alisema Bw Miriti.

Msimamizi huyo wa Afya ya Uzazi Kilifi, amekuwa akiandikisha kupungua kwa visa vya mimba za mapema tangu 2018.Mnamo 2018, visa vya mimba miongoni mwa vijana chipukizi vilikuwa asilimia 33.Idadi hiyo ilishuka 2019 hadi kufikia asilimia 19 kisha 2020 ikawa aslimia 14.

Kufikia sasa Novemba, idadi ya wasichana wajawazito ni asilimia 13.Hata hivyo, alisema Kilifi bado inarekodi kuongezeka kwa visa vya mimba miongoni mwa watoto kutokana na dhuluma za kijinsia tangu 2018.“Katika tafiti nyingi zilizofanywa, wasichana wenye mimba husema kila mara kuwa wao hulazimishwa kushiriki ngono hivyo kusababisha wao kuwa wajawazito,” alisema.

Aliongeza kuwa idadi kubwa ya mimba ni kati ya mtoto na mtoto.“Kinachopaswa kutushughulisha kwa sasa kama kaunti ni kwamba kuna ongezeko la mimba za watoto,” alisemaAlisema serikali ya kaunti ilianzisha mikakati mbalimbali ii kujaribu kudhibiti idadi ya mimba hizo.

Hii ni pamoja na kubuniwa kwa makundi ya marika kwa wasichana ambao wamejifungua katika vituo mbalimbali vya afya.’Mradi huo unafahamika kama Binti kwa Binti unawaleta pamoja wasichana wote ambao wamejifungua ambapo tunawahamasisha kuhusu mbinu salama za kushiriki ngono ili kuwazuia kupata mimba kwa mara ya pili, jinsi ya kuwatunza watoto wao na pia kuwahimiza kurudi shule,” alifafanua.

Aidha, alisema hatua ya serikali kupiga marufuku disco matanga imepunguza mimba za mapema.

You can share this post!

Sh20m kutumiwa kukarabati jengo la makavazi

JAMVI: Ruto anasa ‘samaki’ mkubwa Gavana Mvurya...

T L