Mimi niende Newcastle? Acheni hizo!

Mimi niende Newcastle? Acheni hizo!

NA MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

Supastaa Neymar hana haja na Newcastle United licha ya madai kuwa huenda akaondoka Paris Saint-Germain katika kipindi hiki cha uhamisho.

Mabwanyenye PSG wanafanyia kikosi mabadiliko makubwa baada ya kudhalilishwa na miamba wa Uhispania Real Madrid kwenye Klabu Bingwa Ulaya.

Kocha Mauricio Pochettino alipigwa kalamu wiki moja iliyopita, Luis Campos ni mkurugenzi mpya wa spoti wa PSG na inaonekana Christophe Galtier yumo mbioni kuwa kocha mpya.

PSG inachukua mwelekeo mpya kabisa. Tayari imempa mshambulizi matata Kylian Mbappe mkataba mpya. Tetesi zinadai kuwa kuna uwezekano wa jina kubwa kuhama, huku hali ya baadaye ya Neymar kambini PSG ikiwa haijulikani.

Neymar hatakuwa tena “ndiye kusema” PSG. Mbappe atakuwa sasa na usemi mkubwa, na hiyo huenda ikamaanisha mtu kuondoka. Gazeti la L’Equipe limedai kuwa Neymar ataongezwa kandarasi yake hadi 2027.

Hata hivyo, bado kuna shaka kuhusu kuendelea kwake kuwa uwanjani Parc des Princes. PSG pia haijaeleza msimamo wake kuhusu hali ya Mbrazil huyo. Tatizo kubwa la PSG ni mshahara mkubwa wa Sh96.6 milioni ambao Neymar anapokea kila wiki.

Ni mshahara ambao si klabu nyingi zinaweza kulipa. Ripoti zinadai kuwa mabwanyenye wapya Newcastle United wangependa kusajili Neymar, lakini mwenyewe hajaonyesha ile hamu ya kufanya hivyo.

Wakati huo huo, Manchester United na Brentford zinaaminika kuwa klabu pekee zilizosalia katika vita vya kuwania huduma za kiungo wa Denmark, Christian Eriksen.

Inasemekana zinasubiri tu majibu yake mara atakapokamilisha likizo yake. Alisaini kandarasi ya miezi sita na Brentford ambayo itakatika mwisho wa mwezi huu Juni.

  • Tags

You can share this post!

NYOTA WA WIKI: Victor Osimhen

JAGINA WA SPOTI: Shujaa wa soka ajitolea kukuza chipukizi...

T L