Mimi si mchawi – Raila Odinga

Mimi si mchawi – Raila Odinga

LEONARD ONYANGO na DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga jana aliendeleza juhudi za kuimarisha uhusiano kati yake na viongozi wa kidini huku akisisitiza kwamba hatumii nguvu za kishirikina kujijenga kisiasa kama inavyodaiwa na wapinzani wake.

Kwa miezi miwili sasa, Bw Odinga amekuwa akiendeleza kampeni ya ‘kujitakasa’ dhidi ya madai ya wapinzani wake, hasa Naibu Rais, Dkt William Ruto, ambao humwita ‘mganga’.

Alipozungumza jana akiwa kanisani katika Kaunti ya Busia, alisisitiza kuwa yeye ni Mkristo wa dhati ingawa hapendi kujiganba kuhusu imani yake, tofauti na viongozi wengine wanavyopenda kufanya.

Alipopewa nafasi kuhutubia waumini katika Kanisa Katoliki la St Stephens, Lwanya katika eneo la Mundika, Kaunti ya Busia, alitoa ushuhuda kwamba Mungu amemtendea miujiza mingi maishani mwake hivyo hawezi kuongozwa na nguvu za giza.

Aliwaeleza waumini kuhusu namna Mungu alivyoyanusuru maisha yake baada ya jaribio la mapinduzi ya serikali ya Rais Daniel arap Moi mnamo 1982.

Aliwaambia waumini pia namna alivyotorokea nchini Uganda kupitia Ziwa Victoria huku amevalia mavazi ya kasisi, akaponyoka minyororo ya utawala wa giza kwa nguvu za Mungu.

“Wanaendelea kuniita ‘mganga’. Mimi si mchawi. Huwa ninaenda kanisani mara kwa mara na Mungu amenitendea miujiza mingi,” akasema Bw Odinga aliyebatizwa na kiongozi wa Kanisa la Repentance and Holiness, Dkt David Owuor mnamo 2009.

“Tofauti yangu na wengine ni kwamba mimi sijigambi kuhusu Ukristo wangu. Ninaomba Mungu atusaidie tuunganishe nchi yetu,” akasema Bw Odinga.

Mwezi uliopita, wakati wa hafla ya kumtawaza rasmi Askofu Michael Odiwa kuwa kiongozi wa Parokia ya Homa Bay, Bw Odinga alimtaka Naibu wa Rais kukoma kumrejelea kama mganga.

“Kuna watu wanaoniita mtu wa vitendawili au mganga. Waganga ni watu wanaotibu wagonjwa. Sioni shida yoyote kuitwa mganga lakini nataka mjue kwamba mimi ni Mkristo halisi. Kanisa limehusika pakubwa katika ukombozi wa nchi hii na haki za kibinadamu,” akasema.

Alipokutana na viongozi wa makanisa katika Jumba la Ufungamano jijini Nairobi, mnamo Januari, mwaka huu, Bw Odinga aliwasili akiwa amebeba Biblia kudhihirisha Ukristo wake.

Suala la imani ya Bw Odinga limekuwa likiibuliwa na wapinzani wake kila uchaguzi mkuu unapokaribia. Wapinzani wake wamekuwa wakimhusisha na ushirikina. Katika uchaguzi mkuu wa 2017, wanasiasa wa Jubilee waliokuwa wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, walidai kuwa maneno ya ‘Tibiim’ na ‘Tialala’ yaliyokuwa yakitumiwa na muungano wa NASA kumpigia debe Bw Odinga, yalikuwa na maana fiche ya kishirikina.

Siku chache baada ya Rais Uhuru kutangaza kushirikiana na Bw Odinga, almaarufu handisheki, mnamo 2018, Seneta Maalum Beth Mugo, alionya msanii Joseph Onyango Ochieng’ (Onyi Jalamo) dhidi ya kuingiza jina la Rais kwenye wimbo wake wa ‘Tibiim’.

“Kuna wimbo ambao unahusisha Rais Kenyatta na maneno ‘Tialala’ na ‘Tibiim’. Sisi hatujui maana ya maneno hayo na asili yake. Rais Kenyatta ni Mkristo wala hafai kuhusishwa na maneno hayo,” akasema Bi Mugo alipokuwa akihutubu katika Kanisa la PCEA Runda, Machi 26, 2018.

Hapo jana, Bw Odinga ndiye mwanasiasa pekee aliyeruhusiwa na Padri Moses Langiri kuhutubia waumini ndani ya kanisa hilo huku wengine wakishauriwa kuzungumzia nje ya kanisa baada ya ibada.

“Bw Odinga ndiye mgeni wetu atakayetuhutubia na wengine watazungumzia huko nje baada ya ibada,” akasema Padri Langiri.

Baada ya ibada, Bw Odinga alifanya vikao mbalimbali katika Kaunti ya Busia ambapo alipigia debe mswada wa marekebisho ya katiba, akisema Dkt Ruto ameingiwa baridi ndiposa hataki kutangaza msimamo wake kuhusu kama anaunga mkono au kupinga Mpango wa Maridhiano (BBI).

You can share this post!

Maneja wa Bandari asifu kikosi chake kwa kuzima Ulinzi

Wanaoendeleza ukeketaji Lamu wazimwa