Habari Mseto

Mimi si mdogo jinsi ninavyoonekana, mshtakiwa aambia jaji

May 12th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 18 ameshtakiwa kwa mauaji.

Inadaiwa kwamba Muli Mukonzi alimuua James Mutua Mutuku baada ya kuzozania kidosho.

Alipofikishwa mbele ya Jaji Jessie Lesiit, mshtakiwa alionekana kuwa mwenye umri mdogo.

“Una umri wa miaka migapi? Unaonekana kama wewe ni mtoto. Ulizaliwa mwaka upi?” akauliza Jaji Lesiit.

Jaji Jessie Lesiit aliyeamuru Muli Mukonzi azuiliwe hadi Jumatano, Mei 20, 2020. Picha/ Richard Munguti

Mshtakiwa alijibu na kusema: “Mimi sio mtoto kama ninavyoonekana. Nina umri wa miaka 18. Nilizaliwa Februari 28, 2003. Nilitimiza umri wa miaka 18 mnamo Februari 28, 2020.”

Baada ya kuthibitisha umri wake mshtakiwa alisomewa shtaka na kulikanusha.

Aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka aliomba aruhusiwe hadi Jumatano wiki ijayo awasilishe hati ya kiapo ya kupinga ili mshtakiwa anyimwe dhamana.

Jaji Lesiit aliamuru mshtakiwa azuiliwe katika kituo cha polisi cha Makadara.