Makala

'Mimi sio Rais Paul Kagame, natoka Burundi'

July 14th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

KILA anapopita katika vichochoro mtaani Eastleigh, Nairobi katika shughuli zake za hapa na pale, Maximilien Ndacayisaba hukumbana na jambo ambalo japo amelazimika kulikubali ili kuishi na wakazi vyema, moyoni humkera.

“Kagame, Mheshimiwa, Mtukufu Rais” ni baadhi tu ya majina ambayo anaokutana nao huwa wanamwita. Na japo huwa anaitika, anasema ndani yake huwa anahisi ni kama kukejeliwa.

Maximilien, mwanamume wa umri wa miaka 53, amekuwa nchini tangu 2006 kama mkimbizi, baada ya kutoroka fujo Burundi, ambapo alizaliwa.

“Watu wanafikiri kuwa tuna uhusiano na Rais wa Rwanda Paul Kagame, wanadhani mimi ni wa kutoka Rwanda,” Maximilien ambaye alizungumza na Taifa Leo akasema.

Lakini japo wanaomwita huwa wanadhani ni sifa kwa Maximilien, kwake ni jambo ambalo limekuwa likimwathiri kindani na sasa anasema jina hilo limesababisha jina lake la halisi kusahaulika, na hata yeye mwenyewe kuhisi kama anayeishi maisha ambayo si yake.

“Ningependa watu wajulishwe kuwa mimi si Kagame wala hatuna uhusiano wowote naye. Waambiwe mimi natoka Burundi wala si Rwanda kama inavyodhaniwa. Ningependa Kenya inisaidie kufufua jina langu halisi, watu waambiwe mimi ni Maximilien Ndacayisaba,” akasema.

Aliendelea kusema kuwa hali ya kuitwa jina Kagame imeathiri uhusiano wake na watu; wanaojuana na wengine wasiojuana, mara nyingi kwa mambo ambayo yeye mwenyewe hana uwezo wa kuyarekebisha.

“Watu wafahamishwe kuwa hili jina Kagame ambalo wananiita huwa linaniathiri wakati wowote kunapokuwa na tofauti za kisiasa baina ya Rwanda na taifa jingine. Rais Kagame anapotofautiana na mwenzake kama (Yoweri) Museveni ama (Pierre) Nkurunziza, huwa watu wananiangalia ni kama mimi ni Rais Kagame,” akasema.

Na japo anaishi maisha ya kimaskini mtaani Eastleigh, akifanya kazi za vibarua kupata chakula, wakati mwingine kulala njaa ama nje, jua linapochomoza watu huwa hawajui anayopitia.

“Watu waambiwe mara 1,000 kuwa mimi si tajiri, mimi ni maskini na sijawahi kufanya kazi serikalini. Mimi ni mkimbizi, sina kazi thabiti, sina pa kuishi na hata wakati mwingine nalala njaa. Lakini watu wananiona kama Rais,” Maximilien akaongeza.

Ni maisha haya ya kuanikwa mbele ya umma sana ambayo anasema yamemnyima raha, na kukaribia kumkatisha tamaa maishani.

Hii ni licha ya changamoto za kiafya ambazo amekumbana nazo kwa takriban miaka 25, wakati alitoka Burundi kwa mara ya kwanza na kwenda nchini Amerika kutafuta matibabu.

Mnamo 1994, alikuja nchini Kenya na kuishi kwa miaka miwili kabla ya kwenda Amerika kutafuta matibabu na akarejea mnamo 1996 kwa miezi miwili. Lakini tangu 2006 wakati alitoka Amerika anasema amekuwa jijini Nairobi.

Hata hivyo, alisema hajaweza kupata misaada ambayo wakimbizi hupata, kwa kuwa hana nakala za kuthibitisha kuwa yeye ni mkimbizi.

“Ningependa kupewa hadhi, nitambuliwe kama mkimbizi halisi. Nikipata hicho kitambulisho hata nitaweza kujianzishia biashara niache kuishi hivi,” Maximilien akaambia Taifa Leo.

Alisema kuwa hali hiyo imeathiri uhusiano wake na wanajamii, ikimkosesha upendo na kumfanya kuishi na watu wa kumpotezea heshima.

“Haya si maisha yangu. Watu wanionyeshe upendo kidogo. Kulala kwenye lojing’i, kukosa nyumba na familia katika umri wangu si vyema,” akasema.

Lakini kwa kuwa penye nia pana njia, anasema bado yuko tayari kukusanya vipande vya maisha yake na kufanya juhudi afanye kitu cha kujinufaisha, endapo tu akipewa fursa.

Anasema japo kwa sasa hatambuliwi kama mkimbizi halisi na kuwa amekuwa akihangaishwa na polisi na wakati mwingine kulazimishwa kwenda kuishi kambini Dadaab, akipewa fursa kuishi tena, yuko tayari kabisa.

“Nimechelewa kimaisha lakini bado naweza kufanya kitu na paliposalia. Yote hayajakwisha,” anasema.